51 – Huudhah bin Khaliyfah ametuhadithia: ´Awf ametueleza, kutoka kwa Qasaamah bin Zuhayr ambaye amesema:

“Hana imani yule ambaye hana amana. Hana dini ambaye hana agano.”[1]

52 – Abu Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Mujaahid aliyesema:

“´Ibaadah bora ni rai nzuri.”

53 – Abu Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa Yuusuf bin Maymuun ambaye amesema:

“Nilimwambia ´Atwaa´: “Jopo la watu, ambao tunawazingatia ni wema, kati yetu wanatukemea tunaposema kuwa sisi ni waumini.” ´Atwaa´ akasema: “Sisi ni waislamu waumini. Tuliwakuta Maswahabah wa Mtume wa Allaaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakisema namna hiyo.”[2]

54 – Abu Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa ´Amr bin Murrah, kutoka kwa Abul-Bakhtariy, kutoka kwa Hudhayfah ambaye amesema:

“Kuna aina nne ya mioyo. Moyo ambao ni sahani[3], na huo ni ule moyo wa mnafiki. Moyo uliofungwa[4], na huo ni ule moyo wa kafiri. Moyo ambao ni baridi, kama kwamba ni taa inayowaka, na huo ndio ule moyo wa muumini. Moyo ambao uko na unafiki na imani, mfano wake ni kama mti ambao unamwagiliwa maji mazuri na mabaya; yale yanayoshinda, ndio yameshinda.”[5]

[1] Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh hata kama imekatika. Imekwishatangulia katika namba 7 kupitia kwa Anas, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[2] Cheni ya wapokezi ni dhaifu. Yuusuf bin Maymuun al-Kuufiy as-Swabbaagh ni mnyonge, ndivo alivosema Haafidhw Ibn Hajar.

[3] Umekusanya unafiki na imani. Sahani ina pande mbili; inakutana na makafiri kwa sura moja na inakutana na waumini kwa sura nyingine.

[4] Umewekwa kifuniko kuikubali na kusikiliza haki.

[5] Hadiyth ni Swahiyh kama maneno ya Swahabah.  Layth bin Abiy Sulaym amesimulia tofauti kutoka kwa ´Amr bin Murrah, kutoka kwa Abul-Bakhtariy, kutoka kwa Abu Sa´iyd, kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). 

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 27
  • Imechapishwa: 10/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy