Swali: Ni ipi hukumu ya kumlaani mtu kwa kumlenga?

Jibu: Kilichowekwa katika Shari´ah ni kutolaani isipokuwa kama kuna manufaa ya kufanya hivo. Kwa mfano mtu ambaye analingania katika machafu, anawapiga vita na kuwaua waislamu. Huyu kunaombwa du´aa dhidi yake. Lakini akiwa ni mwenye kuwapa amani basi anaombewa uongofu. Kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu makafiri wa Daws:

“Ee Allaah! Waongoze Daws na walete.”

Aliwaombea du´aa makafiri wa Quraysh:

“Ee Allaah! Mlaani fulani na fulani ambao ndio viongozi wa ukafiri. Ee Allaah! Mlaani fulani mwana wa fulani! Ee Allaah! Mlaani ´Utbah bin Rabi´ah, Shaybah bin Rabiy´ah na Abu Jahl bin Hishaam.”

Kwa sababu walikuwa ndio viongozi wa ukafiri na walinganizi wa ukafiri. Waliwaadhibu waislamu. Kuhusu anayechukia Uislamu lakini anawasalimisha asiombewe dhidi yake. Badala yake anatakiwa kuombewa uongofu.

Hata hivyo ni sawa kumuomba Allaah kwa njia ya jumla kwamba awalaani makafiri, awalaani watenda madhambi na awalaani wezi. Hapana vibaya kuomba kwa njia yenye kuenea. Wakati mtu mmoja alipomlaani yule bwana anayekunywa pombe mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Usimlaani. Kwani hakika anampenda Allaah na Mtume Wake. Usimsaidie shaytwaan dhidi yake.”

Swali: Kwa hivyo kigezo ni kwamba awe anadhihirisha uadui na chuki dhidi ya Uislamu?

Jibu: Anatukana Uislamu au anawapiga vita waislamu.

Swali: Je, alaaniwe muislamu anayelingania katika maovu?

Jibu: Aombewe uongofu na kwamba Allaah awatosheleza kutokana na shari yake. Akiwa ni muislamu basi anaombewa uongofu na kwamba Allaah awatosheleze waislamu kutokana na shari zake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/22573/حكم-لعن-المعين
  • Imechapishwa: 04/07/2023