Kulia kwa mgonjwa na kuelezea maradhi yake kunapingana na Qadar?

Swali: Mimi ni mgonjwa na wakati mwingine hulia kutokana na ilivyogeuka hali yangu baada ya kuugua kwangu. Je, kulia kwangu huku kuna maana ya kupingana na Allaah (Ta´ala) na kutoridhia mipango Yake? Lakini itambulike kuwa kitendo hichi ni chenye kutoka nje ya utashi wangu. Jengine kuzungumza pamoja na ndugu zangu wa karibu kuhusu ugonjwa wangu kunaingia katika mambo hayo?

Jibu: Hakuna neno kulia ikiwa ni kwa kutokwa na machozi peke yake na si kulia kwa sauti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema wakati alipokufa mtoto wake Ibraahiym:

“Hakika macho hutokwa na machozi na moyo huingiwa na huzuni na wala hatusemi isipokuwa yale yenye kumridhisha Mola wetu. “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea. Hakika sisi ni wenye kuhuzunika kwa kutengana na wewe Ibraahiym.”

Zipo Hadiyth nyingi zenye maana kama hii.

Vilevile hakuna ubaya wowote kuwaeleza ndugu na marafiki juu ya maradhi yako na wakati huohuo kumhimdi, kumshukuru Allaah, kumsifu, kumuomba Allaah afya na kufanya zile sababu zilizoruhusiwa.

Tunakuusia kuwa na subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah. Tunakubashiria kheri kwa maneno ya Allaah (Ta´ala):

إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ

“Hakika wale wenye kusubiri watalipwa kikamilifu ujira wao pasi na hesabu.”[1]

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

”Wabashirie wenye kusubiri. Wale ambao unapowafika msiba basi husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” – hao zitakuwa juu yao barakah kutoka kwa Mola wao na rehema na hao ndio wenye kuongoka.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muislamu hapatwi na kutaabika, uzito, maradhi, huzuni, maudhi, dhiki mpaka ule mwiba unaomchoma isipokuwa Allaah humfutia dhambi zake kwayo.”

Vilevile amesema  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule ambaye Allaah anamtakia kheri basi humwonjesha mtihani.”

Tunamuomba Allaah akuponye, afya njema, kutengemaa kwa moyo na kwa matendo. Kwani hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuitikia.

[1] 39:10

[2] 02:155-157

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/144) https://binbaz.org.sa/fatwas/846/%D8%AD%D9%83%D9%85-%D8%A7%D9%84%D8%A8%D9%83%D8%A7%D8%A1-%D8%A8%D8%B3%D8%A8%D8%A8-%D8%A7%D9%84%D9%85%D8%B1%D8%B6-%D9%88%D8%A7%D9%84%D8%AA%D8%AD%D8%AF%D8%AB-%D8%B9%D9%86%D9%87-%D9%85%D8%B9-%D8%A7%D9%84%D8%A7%D8%AE%D8%B1%D9%8A%D9%86
  • Imechapishwa: 30/11/2019