Katika ukurasa wa 236 al-Buutwiy ameandika kichwa cha khabari “Salafiyyah kama madhehebu ni Bid´ah”. Kauli kama hii inasababisha uchanganyikiwaji na mshangao. Vipi ni Bid´ah kuwa na Salafiyyah kama madhehebu na wakati Bid´ah ni upotevu? Vipi itakuwa ni Bid´ah kufuata madhehebu ya Salaf wakati kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah ni wajibu kuifuata na wakati madhehebu haya kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah ni haki na uongofu?

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia awali ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.” (09:100)

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza baada yangu.”

Hivyo ni Sunnah, na sio Bid´ah, kuwa na Salaf kama madhehebu. Hata hivyo, ni Bid´ah kuwa na mfumo wa mtu mwengine.

Ikiwa anamaanisha jina kwa dhati yake ni jipya, kama jinsi alivyosema, na kwamba halikuwa likijulikana hapo mwanzoni, basi ni Bid´ah kwa mtazamo huo. Pamoja na hivyo jina ni kitu sahali. Kosa huko halipelekei katika Bid´ah.

Ikiwa anamaanisha wale wanaojinasibisha na jina hili wanafanya kosa linaloenda kinyume na mfumo wa Salaf, basi anatakiwa kubainisha kosa hilo bila ya kuvamia Salafiyyah.

Kujiita “Salafiy” ni jambo lenye kusifika na jambo zuri ikiwa ina maana kuwa mtu anafuata mfumo wa Salaf na kukemea Bid´ah na ukhurafi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Bayaan li Akhtwaa’ Ba´dhw-il-Kuttaab, uk. 156-157
  • Imechapishwa: 08/11/2022