Swali: Katika nchi za Skandinavia na zilizoko juu waislamu wanapata shida kwa michana kuwa mirefu au mifupi sana. Wakati fulani mchana unaweza kuwa masaa 22 na usiku masaa 2. Katika baadhi ya maeneo jua halizami wala kuchomoza kabisa kwa kipindi cha miezi sita. Ni vipi mtu atafunga katika nchi kama hizi?

Jibu: Shida katika nchi hizo haikufungamana na swawm peke yake bali imefungamana pia na swalah. Lakini ikiwa nchi iko na mchana na usiku, basi inatakiwa kutenda kazi kwa mujibu wa hivo, ni mamoja mchana umerefuka au umefupika. Ama ikiwa michana inakuwa kwa miezi sita na nyusiku inakuwa kwa miezi sita, basi watu hawa wanatakiwa kukadiria wakati wa funga zao na swalah zao. Lakini watategemea kitu gani? Baadhi ya wanazuoni wamesema kuwa watahesabu kwa kutegemea wakati wa Makkah, kwa sababu Makkah ndio msingi wa miji unaofatwa. Wengine wakasema kuwa wanatakiwa kufuata mji wa kati na kati ambapo mchana ni masaa 12 na usiku ni masaa 12. Wako wanazuoni vilevile waliosema kuwa wanatakiwa kufuata mji ulio karibu zaidi na wao ambao wana mchana na usiku wa kawaida. Haya ndio maoni yenye nguvu. Wana haki zaidi ya kufuata ule mji ambao uko karibu zaidi na wao kijiografia. Kujengea juu ya haya wanatakiwa kutazama ile nchi ambayo iko na mchana na usiku na wafuata wakati wake inapokuja katika swalah, funga na mengineyo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/321-322)
  • Imechapishwa: 01/05/2021