Kufasiri Aayah zilizo wazi pasina kurejea kwenye vitabu vya tafsiri ya Qur-aan

Swali: Ni ipi hukumu ya kufasiri Aayah ya Qur-aan kwa udhahiri wake, bi maana kwa maana ambayo inafahamika na watu wote bila ya kurejea katika [vitabu vya] tafsiyr ya Qur-aan vya wanachuoni?

Jibu: Hapana, haijuzu. Mambo ya dhahiri kama mfano wa swalah, swawm, Pepo na Moto, matishio ya adhabu, ni sawa kwa kuwa yanafahamika na watu wa kawaida. Kuhusiana na hukumu za Kishari´ah, kuhalalisha na kuharamisha, mambo maalum na ya jumla, yasiyofungamana na yaliyofungamana, [Aayah] iliyofuta na [Aayah] iliyofutwa, haya ni mamo yenye kufahamika tu na wale waliobobea katika elimu. Haijuzu kuifasiri Qur-aan hivi hivi tu. Ama kuhusu mambo ya dhahiri, kukitajwa Moto unaujua, kukitajwa Pepo unaijua, kukitajwa matendo mema unayajua, kukitajwa swalah unaijua. Kwa mfano:

حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ

“Shikamaneni na swalah.” (02:238)

Sio lazima urejee kwenye vitabu vya tafsiyr ya Qur-aan na kuangalia ni nini swalah. Waislamu wanazijua. Kuna mambo yanayojulikana na wasiokuwa wasomi. Kuna mambo yanayojulikana na wanachuoni. Kuna mambo yasiyojulikana na yeyote isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tafsiyr al-Mufasswal (76) http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/tf–1432-11-12.mp3
  • Imechapishwa: 22/08/2020