Kuchelewesha swalah kwa sababu ya kazi ya kijeshi

Swali: Mimi ni mtu ninayefanya kazi ya kijeshi. Wakati mwingine nalazimika kuchelewesha swalah nje ya wakati wake kama mfano wa ´Aswr na siwezi kuasi. Mwenye kuasi anaadhibiwa kwa kufukuzwa au kufungwa na mfano wa hayo.

Jibu: Haifichikani kwamba swalah ndio nguzo ya Uislamu na kuwa ni nguzo ya pili miongoni mwa nguzo zake tano na kwamba kuiswali ndani ya wakati wake ni miongoni mwa sharti zake muhimu zaidi na kwamba kumtii kiumbe katika maasi ni kitu kisichofaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika si venginevyo utiifu unakuwa katika mema.”

 Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba.”

Ukishayajua haya basi inakulazimu kuswali ndani ya wakati wake na kutoichelewesha. Lakini inafaa wakati wa haja kubwa kukusanya kati ya Dhuhr na ´Aswr katika wakati wa kimoja wapo na kati ya Maghrib na ´Ishaa katika wakati wa kimoja wapo. Kama vile msafiri, mgonjwa na watu mfano wao.

Ama kuichelewesha ´Aswr mpaka jua linageuka manjano au ´Ishaa mpaka baada ya nusu ya usiku ni jambo halijuzu kwa hali yoyote.

Ni lazima kwenu kutilia umuhimu jambo hili na wasilisheni barua yangu hii kwa wasimamizi wenu. Nao – Allaah akitaka – watatekeleza yale yanayoafikiana na Shari´ah. Wasipotekeleza basi tufahamisheni na sisi – Allaah akitaka – tutawasiliana na mamlaka zinazohusika kuchukua hatua inayofaa.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/381)
  • Imechapishwa: 01/10/2021