Kigezo cha anayemrisha mema na kukemea maovu

Swali: Ni vigezo vipi vya kuamrisha mema na kukataza maovu ili nguzo hii kubwa itekeleze ujumbe wake, kwa sababu baadhi ya watu hutumia mpaka inageuka kufanana na yale ya Mu´tazilah na Khawaarij?

Jibu: Kanuni zake zinajulikana. Hatakiwi kusema kama wanavyosema Khawaarij na Mu´tazilah kwamba maasi ni ukafiri na upotofu na kwamba mwenye kufanya maasi ni kafiri. Hapana, mwenye kufanya maasi yuko katika khatari, lakini si kafiri muda wa kuwa ni mwenye kumwabudu Allaah pekee, ni muislamu, anamwamini Allaah na siku ya Mwisho, anaharamisha aliyoharamisha Allaah na anahalalisha aliyohalalisha Allaah na anawajibisha aliyowajibisha Allaah, lakini huweza kutokea kwake kosa na madhambi. Kwa hiyo wajibu ni kuyakataza kwa hekima na mawaidha mazuri na amfafanulie hukumu yake ikiwa ni mjinga na ashikwe mikono yake. Akiendelea katika hilo basi aadhibiwe kwa adhabu anayostahiki zaidi na kadhalika. Ikiwa amefanya kosa linalopelekea kutekelezewa adhabu za Allaah, basi itekelezwe juu yake, kama mwizi hukatwa na mzinifu hupigwa mijeledi ikiwa hajaoa na hufukuzwa mwaka mmoja. Ikiwa ameoa, basi hupigwa mawe. Kila jambo lina mpaka wake na mwenye kulifanya hupata anachostahiki. Kwa hiyo mambo kanuni zake zinajulikana. Ukafiri una hali yake na maasi yana hali yake. Maovu ni tofauti na yana ngazi zake. Kuyakataza hutofautiana kwa mujibu wa uovu wake na ukubwa wake. Adhabu zake ni tofauti. Ni lazima yule anayeamrisha na anayekataza awe juu ya ujuzi, kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi.”[1]

Ni lazima awe juu ya ujuzi katika anachoamrisha na anachokataza, ajifunze na afahamu dini. Asizungumze katika dini bila elimu. Asiwe anakataza wala kuamrisha isipokuwa kwa ujuzi na elimu. Ama mwenye elimu basi ni wajibu wake aseme, atoe maelekezo na awasaidie wanaosimama juu ya haki na wala asighafilike wala asinyamaze.

[1] 12:108

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/2197/بيان-ضوابط-الامر-بالمعروف-والنهي-عن-المنكر
  • Imechapishwa: 18/07/2026