Kauli yenye nguvu juu ya mwenye kuacha swalah

Swali: Sisi ni vijana ambao tumetofautiana juu ya masuala kuhusu swalah. Ni ipi hukumu ya mwenye kuacha swalah moja kwa moja? Je, atadumishwa Motoni milele? Ni ipi hukumu vilevile kwa mwenye kuacha swalah mara kadhaa na anaswali mara kadhaa. Je, huyu anazingatiwa kuwa ni katika makafiri na katika watakaodumishwa katika Moto?

Jibu: Mwenye kuacha Swalah amekufuru, sawa ikiwa ameacha kikamilifu au baadhi yake. Hii ndio kauli ya sawa katika kauli za wanachuoni hata kama hatokanusha uwajibu wake. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ

“[Watawauliza]: “Ni kipi kilichokuingizeni katika [Moto wa] Saqar?” Watasema: “Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali.” (74:42-43)

Watasema jambo la kwanza kwamba sio miongoni mwa wanaoswali. Amesema Mtume Mtukufu (´alayhis-Swalaatu was-Salaam):

“Baina ya mtu na kufuru na shirki ni kuacha swalah.”

Maana hapa ni kufuru na shirki kubwa. Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ahadi iliyopo baina yetu na wao ni swalah, mwenye kuiacha basi amekufuru.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kichwa na nguzo ya Uislamu ni swalah.”

Mwenye kuiacha moja kwa moja, kufuru yake iko wazi. Ikiwa anaswali wakati fulani na anaacha wakati mwingine, hali kadhalika ni kafiri. Hii ndio kauli ya sawa. Ama akikanusha uwajibu wake na kusema “Sio wajibu kuswali”, huyu ni kafiri kwa makubaliano ya watu wote. Akikanusha uwajibu wake hata kama ataswali na kusema “Sio wajibu”, ni kafiri kwa makubaliano ya wanachuoni wote hata kama ataswali. Ama mwenye kukubali uwajibu wake lakini akapuuzia kuswali, huyu ndiye wanachuoni wametofautiana. Maoni sahihi ni kwamba anakufuru kwa hilo hata kama atakubali uwajibu wake. Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefungamanisha ukafiri kwa kule kuiacha na wala hakuufungamanisha ukafiri kwa kukanusha uwajibu wake. Amesema wazi:

“Baina ya mtu na kufuru na shirki ni kuacha swalah.”

Amesema tena (´alayhis-Salaam):

“Mwenye kuacha swalah ya ´Aswr, matendo yake yameporomoka.”

Amesema tena (´alayhis-Salaam):

“Ahadi iliyopo baina yetu na wao ni swalah, mwenye kuiacha basi amekufuru.”

Kukufurishwa kwake kumewekwa wazi hata kama hakukanusha uwajibu wake na tunamuomba Allaah afya.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://subulsalam.com/play.php?catsmktba=12825
  • Imechapishwa: 20/11/2014