Je, nyoka na nge wanauliwa na mswaliji bila ya kuwaonya?

Swali: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoamuru kuua viumbe wawili wenye madhara, nyoka na nge, hata akiwa mtu yuko ndani ya swalah. Je, agizo hili linahusu hata nyoka wa ndani ya nyumba ambao si wenye alama mbili kichwani wala wale vipofu, bila ya onyo, au linahusiana na wale tu waliokwishaonywa?

Jibu: Inawezekana kuwa agizo hili limefuta hukumu ya Hadiyth ya Abu Sa´iyd. Ufafanuzi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu viumbe hawa watano[1] na wengineo wenye madhara unatoa uwezekano kuwa hukumu ya kuonya nyoka wa ndani ya nyumba imefutwa na sasa nyoka wote wa aina hii wanaruhusiwa kuuawa bila onyo. Pia kuna uwezekano kwamba hukumu hii bado ni yene kufanya kazi na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikusudia nyoka ambao si wa ndani ya nyumba, kama wale wanaopatikana misikitini, barabarani au porini, hawa wanapaswa kuuawa moja kwa moja. Ama nyoka wa ndani ya nyumba, wao wanapaswa kuonywa mara tatu kabla ya kuuawa. Wakirejea wanauliwa, kama Hadiyth inavosema:

”Hakika nyumba hizi zina majini ambao wanaweza kujidhihirisha kwa sura ya nyoka. Kwa hiyo haifai kuuawa hadi waonywe mara tatu.”

Swali: Je, nyoka waonywe mara tatu hata kama ni ndani ya siku moja?

Jibu: Hata kama ni ndani ya siku moja. Katika baadhi mapokezi yanaeleza mara tatu na mengine siku tatu na mengine tatu. Muhimu ni kwamba onyo lifanywe mara tatu, ni mamoja iwe ni ndani ya siku moja au siku tofauti.

Swali: Je, kilicho sahihi zaidi ni kwamba nyoka wa ndani ya nyumba wanatengwa kutoka kwa agizo hili la jumla?

Jibu: Kilicho karibu zaidi na msingi wa Shari´ah ni kwamba kilicho maalum kinachukua nafasi ya kilicho cha jumla. Hivi ndivo inavosema kanuni.

[1]  Nyoka, nge, panya, mbwa mwitu na kunguru.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/24977/هل-تقتل-الحية-والعقرب-في-الصلاة-بغير-انذار
  • Imechapishwa: 19/01/2025