Je, ni lazima kwa muislamu kuyafanya Tayammum juu ya kila swalah?

Swali: Je, ni lazima kwa mtu kufanya Tayammum juu ya kila swalah au inafaa kwake kuswali zile swalah za faradhi na zilizopendekezwa azitakazo muda wa kuwa hajapatwa na hadathi baada ya Tayammum?

Jibu: Inafaa kwa muislamu pindi anapofanya Tayammum inayokubalika katika Shari´ah akaswali kwa Tayammum hiyo faradhi na swalah za sunnah azikatazo maadamu amekosa maji au ameshindwa kuyatumia muda wa kuwa hajapatwa na hadathi au hajapata maji kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Allaah (Subhaanah) amesema:

فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ ۚ مَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ وَلَـٰكِن يُرِيدُ لِيُطَهِّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“… kisha hamkupata maji, basi fanyeni Tayammum kwa ardhi ilio safi panguseni kwayo nyuso zenu na mikono yenu. Allaah hataki kukufanyieni magumu, lakini anataka kukutwaharisheni na akutimizieni neema Yake juu yenu ili mpate kushukuru.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ardhi kwangu mimi imefanywa kuwa mahali pa kuswalia na yenye kutwahirisha. Mtu yeyote kutoka katika Ummah wangu ambaye utafika wakati wa swalah basi yuko na msikiti na kitu cha kumtwahirisha.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mchanga ni wudhuu´ wa muislamu ijapo hatopata maji miaka ishirini. Akipata maji basi amche Allaah na ayagusishe ngozi yake.”

Zipo Hadiyth nyingi juu ya jambo hilo.

[1] 05:06

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/203)
  • Imechapishwa: 04/09/2021