Je, kuna matamshi ya nia ya swawm?

Swali: Je, kuna matamshi ya nia ya swawm? Je, inafaa kuyatamka kwa sauti ya juu? Je, kuna du´aa wakati wa kufungua swawm? Je, inafaa kuitamka kwa sauti ya juu?

Jibu: Hakuna matamshi kwa ajili ya nia ya swawm. Sahihi ni kwamba asitamke nia kwa sauti ya juu katika ´ibaadah yoyote kukwemo hajj. Wale wenye kusema kuwa nia katika hajj inatakiwa kutamkwa kwa sauti ya juu hawakuleta dalili isipokuwa yale yaliyopokelewa kuhusu yule mtu aliyesema:

“Nimekuitikia Allaah kutoka kwa Shubrumah.”

Inawezekana kuwa alisema hivo kwamba amehiji kwa niaba ya Shubrumah, kwa sababu maana ya hajj ni kule kukusudia. Inawezekana vilevile ya kwamba amesema hivo kwa maana ya kuwa anamuwekea manuizi Shubrumah. Kwa hivyo kunasemwa kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kuhusu du´aa wako wanazuoni wanaosema kuwa imethibiti Hadiyth ifuatayo:

ذَهَبَ الظَّمَأُ وَابْتَلَّتِ الْعُرُوقُ وَثَبَتَ الْأَجْرُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ

“Kiu kimeondoka, mishipa imerowana na ujira umepatikana – Allaah akitaka.”[1]

Kinachodhihiri ni kwamba hakukuthibiti Hadiyth yoyote maalum katika kuomba. Vinginevyo imethibiti kwamba mfungaji anayo du´aa yenye kuitikiwa wakati wa kukata kwake swawm. Kwa hivyo mwombe Allaah msamaha, akuponye na mambo mengine unayohitaji.

[1] Abu Daawuud (2357), al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (4/239) na katika ”as-Sunan as-Sughraa” (1390) na ad-Daaraqutwniy (240). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl”.

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaaih wa Naswaaih, uk. 74
  • Imechapishwa: 15/03/2024