Swali 33: Shubuha ya nne wanasema kuwa wao wanachukia Bid´ah lakini hawawajengei chuki wazushi, kwa sababu chuki haipelekei katika uadui. Unaweza kumchukia mtu lakini usimfanyie uadui. Dalili yao wanasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kuhusu baadhi ya wanafiki waliokuwa wanataka kukutana naye:

”Mwache aingie. Ni ndugu mbaya aliyoje!”[1]

Wakati mnafiki huyu alipoingia akamuonyesha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) uso wa bashasha. Kitendo cha yeye kumchukia na akamuonyesha uso wa bashasha ina maana ya kwamba hakumjengea uadui. Unasemaje juu ya utata huu?

Jibu: Utata huu ni dhaifu. Wao wanakubali kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimchukia. Chuki inakuwa wapi? Moyoni au mdomoni? Chuki inakuwa moyoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumpa maneno makali. Sisi hatusemi kuwa mtu azungumze na Ahl-ul-Bid´ah kwa ukali. Zungumza nao kwa hekima, maneno mazuri na kujadiliana nao kwa njia nzuri zaidi. Huu ndio mfumo bora wakati wa kuwalingania Ahl-ul-Bid´ah na wengineo kama makafiri, watenda madhambi na wajinga. Tunawalingania kwa hoja na dalili, hekima na mawaidha mazuri. Ikiwa pamoja na hilo mzungumzaji atawaonyesha tabia nzuri inakuwa ni rahisi kwa mzushi huyu, mjeuri na muulizaji huyu kurejea katika haki. Baadhi wanarejea katika Uislamu na mzushi na mtenda dhambi anajirejea katika upindaji wake – ikiwa Allaah anamtakia kheri.

[1] Ahmad (6/38), al-Bukhaariy (6032) na Muslim (2591).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kashf-us-Sitaar, uk. 67-68
  • Imechapishwa: 09/11/2022