Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

41 – Muhammad ni mja Wake aliyeteuliwa, Nabii Wake aliyechaguliwa na Mtume Wake aliyeridhiwa.

MAELEZO

Wakati Shaykh (Rahimahu Allaah) mwanzoni mwa maneno yake alipomaliza kubainisha katika kijitabu chake yale ambayo inapasa kuyatambua katika utambuzi juu ya Allaah (Subhaanah), kuamini kuwa Yeye ndiye Mola anayestahiki kuabudiwa pasi na mwingine na kwamba anasifika kwa sifa kamilifu na tukufu ambazo anasifika nazo milele na daima, ndipo akaenda katika yale ambayo inalazimika kuyaamini kuhusu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema:

“Muhammad ni mja Wake aliyeteuliwa… “

Ni lazima kuyaitakidi haya. Kama ambavyo tunashuhudilia uungu wa Allaah, vivyo hivyo tunashuhudilia ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Namna hiyo shahaadah mbili zinakuwa zenye kulazimiana.

Jina la Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) limetajwa ndani ya Qur-aan:

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii. Na Allaah daima kwa kila kitu ni Mjuzi.”[1]

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَآمَنُوا بِمَا نُزِّلَ عَلَىٰ مُحَمَّدٍ وَهُوَ الْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ ۙ كَفَّرَ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَأَصْلَحَ بَالَهُمْ

”Wale walioamini na wakatenda mema na wakaamini yale aliyoteremshiwa Muhammad, nayo ni ya haki kutoka kwa Mola wake atawafutia maovu yao na atatengeneza hali zao.”[2]

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّهِ

“Muhammad ni Mtume wa Allaah.”[3]

Anayo majina yake mengine yamepokelewa katika Sunnah ambayo yametajwa na Ibn-ul-Qayyim katika “Jalaal-il-Afhaam”.

[1] 33:40

[2] 47:2

[3] 48:29

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 56-57
  • Imechapishwa: 09/11/2022