Inajuzu kufanya I´tikaaf katika misikiti isiyokuwa mitatu?

Swali: Inajuzu kufanya I´tikaaf katika misikiti isiyokuwa mitatu?

Jibu: Inajuzu kufanya I´tikaaf katika misikiti isiyokuwa mitatu ambayo ni msikiti Mtakatifu, msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na msikiti wa al-Aqswaa. Dalili ya ueneaji huo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ ۗ تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ فَلَا تَقْرَبُوهَا ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ آيَاتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ

“Na wala msichanganyike nao hali ya kuwa nyinyi ni wenye kukaa I’tikaaf  misikitini. Hiyo ni mipaka ya Allaah, hivyo basi msiikaribie. Hivyo ndivyo Allaah anavyobainisha Aayah Zake kwa watu ili wapate kumcha.”[1]

Ayaah hii inawazungumzisha waislamu wote. Ikiwa tutasema kuwa makusudio ni ile misikiti mitatu basi tutasema kuwa waislamu wengi hawasemezwi na Aayah hii. Waislamu wengi wako nje ya Makkah, al-Madiynah na Yerusalemu. Kwa ajili hii tunasema kuwa inafaa kufanya I´tikaaf katika misikiti yote. Lau Hadiyth:

“Hakuna I´tikaaf isipokuwa katika misikiti mitatu.”

itakuwa ni Swahiyh basi tunasema kuwa kinachokusudiwa ni kwamba hakuna I´tikaaf ambayo ni kamilifu na bora zaidi isipokuwa katika ile misikiti mitatu. Hapana shaka ya kwamba kufanya I´tikaaf katika ile misikiti mitatu ni bora kuliko kufanya kwenye mingine kama ambavyo kuswali kwenye misikiti hii mitatu ni bora kuliko kuswali kwenye mingine. Swalah  moja katika msikiti Mtakatifu ni bora kuliko swalah laki moja kwenye misikiti mingine, swalah moja katika msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni bora kuliko swalah elfu moja kwenye misikiti mingine na swalah moja katika msikiti wa al-Aqswaa ni bora kuliko swalah mia tano kwenye misikiti mingine.

[1] 02:186-187

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (20/160-161)
  • Imechapishwa: 16/06/2017