Swali: Kuna imamu wa msikiti nimemsikia akisoma Hadiyth mwezi huu akizungumzia juu ya fadhila za Qur-aan. Katika maneno yake alisema kuwa Qur-aan ameitengeneza/ameiumba Allaah. Katika kupitia kwangu shule katika somo la Tawhiyd nimepata kujua kuwa Mu´tazilah ndio wenye kusema kuwa Qur-aan imeumbwa na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameziponda ponda hoja zao. Kwa sababu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini kuwa Qur-aan haikuumbwa, bali ni maneno ya Allaah ya kihakika ambayo yameteremshwa kutoka Kwake kumpelekea nayo Muhammad. Mimi sijui kama Shaykh alikuwa na makusudio mengine aliposema hivo au vipi? Unaonaje kuhusiana na maneno aliyosema imamu huyu katika msikiti huyo? Naomba uniwekee wazi.

Jibu: Ikiwa mambo ni kama unavyoamini ya kwamba unaitakidi kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah ambayo amezungumza kihakika na akamteremshia nayo Muhammad, wewe ni katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, upande mwingine imamu wa msikiti amesema kuwa Qur-aan ameitengeneza Allaah, wewe ndiye una ´Aqiydah sahihi inapokuja katika Maneno ya Allaah. ´Aqiydah yako inaafikiana na yale wanayoamini Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Kuhusiana na maneno ya imamu aliposema kuwa Qur-aan imetengeneza Allaah amekosea kwa kuwa yanaenda kinyume na dalili ya Qur-aan na Sunnah na mfumo wa Salaf katika kuvifahamu. Unaweza kuwasiliana naye na kumzindua. Pengine alisema hivo kwa kuteleza ulimi bila ya kukusudia. Hivyo ajisahihishe na atamke usawa.

Baada ya kuzungumza naye ukiona kuwa anaitakidi kuwa Qur-aan imeumbwa na akaendelea katika I´tiqaad hiyo, mwelekeze katika haki ukiwa na uwezo huo. Vinginevyo mpe kitabu “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah” na “at-Tadmuriyyah” vya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) na kitabu “Sharh at-Twahaawiyyah” cha Ibn Abil-´Izz (Rahimahu Allaah). Unaweza vilevile kumwelekeza katika vitabu hivyo akavisome ili aijue ´Aqiydah sahihi.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (3/152)
  • Imechapishwa: 23/08/2020