Imamu mkubwa na Haafidhw wa zama zake Misri; Abu Ja´far al-Miswriy. Alikuwa akitambulika kwa at-Twabariy.

Baba yake alikuwa mwanajeshi Twabaristan.

Abu Ja´far alikuwa ni kiongozi katika suala hili na ni mara chache macho yanaona mfano wake, pamoja uaminifu na kumcha kwake Allaah.

Kwa mujibu wa Ibn Yuunus alizaliwa mwaka 170.

Baadhi ya wale ambao amehadithia kutoka kwao ni pamoja na Ibn Wahb, Sufyaan bin ´Uyaynah, ´Abdur-Razzaaq, Asad bin Muusa, Abu Nu´aym na wengineo.

Miongoni mwa wale wamehadithia kutoka kwake ni pamoja na al-Bukhaariy, Abu Daawuud, Abu Zur´ah ar-Raaziy, Muhammad bin Yahyaa, an-Nasaa´iy na wengineo.

Muhammad bin ´Abdillaah bin Numayr amesema:

“Hakuna yeyote aliyekuja kwetu ambaye ni bingwa wa Hadiyth kutoka Hijaaz kama kijana huyu – akikusudia Ahmad bin Swaalih.”

Abu Zur´ah ad-Dimashqiy amesema:

“Nilifika ´Iraaq, Ahmad bin Hanbal akaniuliza: “Ni nani uliyemwacha Misri?”Nikasema:

”Ahmad bin Swaalih.”Ndipo akafurahi, akatabasamu, akamsifu na akamwombea kwa Allaah.”

Abul-Hasan al-Harawiy amesema:

“Nilimuuliza Ahmad bin Hanbal: “Ni nani mjuzi zaidi wa Hadiyth za az-Zuhriy?” Akasema: “Ahmad bin Swaalih na Muhammad bin Yahyaa an-Niysaabuuriy.”

Ya´quub bin Sufyaan amesema:

“Niliandika kutoka kwa Mashaykh elfu ambao ni waaminifu lakini hakuna yeyote katika wao ambaye naona kuwa ni hoja mbele ya Allaah isipokuwa Ahmad bin Swaalih Misri na Ahmad bin Hanbal ´Iraaq.”

al-Bukhaariy amesema:

“Ahmad bin Swaalih ni mwaninifu na mwaminiwa. Sijamuona yeyote anayemzungumza kwa ubaya kwa hoja. Ahmad bin Hanbal, ´Aliy, ´Umayr na wengine wanamsifu Ahmad bin Swaalih. ´Aliy alikuwa akisema: “Muulize Ahmad, hakika yeye ni imara.”

Ahmad bin Swaalih amesema:

“Niliandika Hadiyth 100.000 kutoka kwa Ibn Zabaalah. Kisha baadaye ikanibainikie kuwa ni mwenye kutunga Hadiyth na hivyo nikaziacha Hadiyth zake.”

Ahmad al-´Ijliy amesema:

“Ahmad bin Swaalih ni mmisri mwaminifu na mwenye kufuata Sunnah.”

Abu Haatim amesema:

“Ni mwaminifu. Nimeandika kutoka kwake Misri, Dameski na Antaakiyah.”

al-Khatwiyb amesema:

“Nimefikiwa na khabari kwamba Ahmad bin Swaalih alikuwa hapokei Hadiyth isipokuwa tu kutoka kwa watu waliomea ndevu. Hawaachi vijana kuhudhuria vikao vyake. Siku moja Abu Daawuud as-Sijistaaniy akaja na mwanae ili asikie kutoka kwake. Mwanae alikuwa bado kijana na hajamea ndevu, jambo lililofanya Ahmad bin Swaalih akamsomea Abu Daawuud kuja na mtoto wake. Abu Daawuud akamwambia: “Hata kama ni mdogo ni mwenye kuhifadhi zaidi kuliko wenye ndevu. Mpe mtihani kwa ukitakacho!” Ndipo akaanza kumpa mtihani mtoto wa Abu Daawuud ambapo akajibu yale yote aliyomuuliza. Matokeo yake akamwacha kukaa katika vikao vyake na hakukuweko kijana mwingine aliyekuwa akihudhuria zaidi yake.”

al-Bukhaariy na Ibn Zabr wamesema:

“Ahmad bin Swaalih alikufa Dhul-Qa´dah mwaka 248.”

Abu Daawuud amesema:

“Nilimuuliza Ahmad bin Swaalih kuhusu yule mwenye kusema kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah na hasemi kuwa imeumbwa wala haikuumbwa. Akasema “Mtu kama huyo ni mwenye mashaka na mwenye mashaka ni kafiri.”

Amesema tena:

“Mwenye kusema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumwa ni kafiri.”

Akisema matamshi ya Qur-aan yameumbwa na akakusudia Qur-aan, ni sahihi kwamba ni kafiri, na ikiwa anakusudia kule kutamka kwa midomo, sauti na kitendo, basi mwenye kupatia. Allaah (Ta´ala) ndiye Muumbaji wetu na Yeye ndiye ameumba matendo yetu.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (12/160-178)
  • Imechapishwa: 23/09/2020