Ibn ´Uthaymiyn kukusanya Maghrib na ´Ishaa kipindi cha majira ya joto

Swali: Baadhi ya miji mawingu mekundu yanachelewa kupotea ambayo kwayo ndio unaingia wakati wa ´Ishaa na inakuwa ni vigumu kwao kuisubiri. Wafanye nini?

Jibu: Ikiwa mawingu mekundu hayapotei mpaka kuchomoza kwa alfajiri au yanapotea kwa kipindi kifupi kiasi cha kwamba mtu hawahi kuiswali ´Ishaa kabla ya kuchomoza kwa alfajiri, basi watu hawa hukumu yao ni kama ya wale wasiokuwa na ´Ishaa. Kwa hivyo watatakiwa kukadiria wakati wake kutegemea na nchi iliokaribu zaidi kwao ambao wana wakati wa ´Ishaa unaokubaliwa. Yapo maoni mengine yanayosema kuwa wanatakiwa kutazama muda wa Makkah.

Ikiwa mawingu mekundu yanapotea kabla ya kuchomoza kwa alfajiri kwa muda mrefu ambao wanaweza kuiswali ´Ishaa, basi wanatakiwa kusubiri mpaka yapotee mawingu hayo.

Isipokuwa ikiwa kama kusubiri kunakuwa kugumu kwao. Basi katika hali hiyo inafaa kwao kukusanya kati ya Maghrib na ´Ishaa wakati wa Maghrib. Kufanya hivi ni kwa sababu ya kuondosha uzito na ugumu. Allaah (Ta´ala) amesema:

يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

“Allaah anakutakieni mepesi na wala hakutakieni mazito.” (02:185)

وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ

“Hakukufanyieni ugumu wowote ule katika dini.” (22:78)

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim imepokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikusanya kati ya Dhuhr na ´Aswr na kati ya Maghrib na ´Ishaa al-Madiynah pasi na khofu wala mvua.” Wakasema: “Nini ilikuwa malengo yake?” Akasema: “Alikuwa hataki kuupa uzito Ummah wake.”

Bi maana ili wasipate uzito wa kuacha kukusanya.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/206-207)
  • Imechapishwa: 03/08/2020