Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

وعن أبي يَزيدَ مَعْنِ بنِ يَزيدَ بنِ الأخنسِ رضي الله عنهم وهو وأبوه وَجَدُّه صحابيُّون قَالَ: كَانَ أبي يَزيدُ أخْرَجَ دَنَانِيرَ يَتَصَدَّقُ بِهَا، فَوَضعَهَا عِنْدَ رَجُلٍ في الْمَسْجِدِ، فَجِئْتُ فأَخذْتُها فَأَتَيْتُهُ بِهَا. فقالَ: واللهِ، مَا إيَّاكَ أرَدْتُ، فَخَاصَمْتُهُ إِلى رسولِ اللهِ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ: ((لكَ مَا نَوَيْتَ يَا يزيدُ، ولَكَ ما أخَذْتَ يَا مَعْنُ)). رواهُ البخاريُّ

5 – Abu Yaziyd Ma’ni bin Yaziyd bin al-Akhnas (Radhiya Allaahu ‘anhum) – yeye, baba yake na babu yake walikuwa ni Maswahabah – amesimulia: “Baba yangu Yaziyd alikuwa ametoa dinari akizitolea swadaqah. Akaziweka kwa bwana mmoja msikitini ambapo nikaja na kuzichukua na nikaja nazo. Akaniambia: “Naapa kwa Allaah sikuwa nimekukusudia wewe” nikashtakiana naye kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ambapo akasema: “Ee Yaziyd, utapata ulichokinuia, na ee Ma’ni, ni chako ulichokichukua.”[1]

Miongoni mwa faida za Hadiyth hii ni kwamba inajuzu kwa mtu kumpa zakaah mwanae kwa sharti isiwe kwa kufanya hivo anataka kudondosha wajibu ulio juu yake. Kwa mfano mtu yuko na zakaah na anataka kumpa mwanae ili asimuombe matumizi, basi zakaah hii haitoshelezi na haisihi. Amekusudia kwa kumpa kwake zakaah kuvunja wajibu wa kuhudumia. Lakini hata hivyo akimpa kwa ajili ya kumlipia deni alilonalo, kwa mfano mtoto ana shida na baba yake akampa katika zakaah yake ili kumlipia gharama hii, hili ni sawa na linatosheleza katika zakaah. Mtoto wake ndio mtu wa karibu zaidi kwake. Kwa kitendo hichi hakukusudia kuvunja wajibu ulio juu yake. Alichokusudia ni kulipa deni la mtoto wake na sio matumizi yaliyo juu yake. Ikiwa haya ndio makusudio yake, basi zakaah ni halali kwake.

[1] al-Bukhaariy

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/41)
  • Imechapishwa: 22/01/2023