Swali: Tunataraji kutoka kwa Shaykh wetu kutuwekea wazi Hadiyth na Aayah kuhusu kufunika uso na vitanga vya mikono pamoja na kuzifafanua na kubainisha dalili kwa undani. Tumesikia kwa wanachuoni wengi ya kwamba wanachuoni wengi wanaonelea kujuzu kuonesha uso na vitanga vya mikono na wanatumia dalili Hadiyth ya Asmaa´ pindi alipoingia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Ewe Asmaa´! Mwanamke anapofikia umri wa kupata hedhi, asioneshe kitu isipokuwa hili na hili – akaashiria uso na vitanga.” Wanatumia hoja vile vile tafsiri ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kuhusu Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

“Na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika.” (24:31)

Maana ya “… yale yanayodhihirika” kunakusudiwa uso na vitanga. Akasema hii ni dalili ya kujuzu kuonesha uso na vitanga. Tunaomba utupe faida.

Jibu: Masuala haya wamevutana kwayo wanachuoni (Rahimahumu Allaah). Kauli sahihi ni kuwa, uso na vitanga ni ´Awrah. Na uso ni khatari zaidi, kwa kuwa ndipo kulipo uzuri wote wa mwanamke. Na (uso) unaingia katika Kauli Yake (Ta´ala):

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ

“Na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao… ” (24:31)

Dalili kuhusu hili (kufunika uso) ni nyinngi, miongoni mwazo ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ

“Na mnapowauliza (wake zake) haja, waulizeni nyuma ya pazia. Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao.” (33:53)

Na hili ni kwa jumla na Allaah Hakubagua kitu, sawa vitanga, uso na visivyokuwa hivyo. Kwa kuwa inaonesha dalili ya ujumla. Kisha Akasema (Subhaanah) kutokana na maslahi inayopati-kana kwa watu wote:

ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ

“Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao.”

Ni dalili ioneshayo kuwa Hijaab ni utwaharifu kwa nyoyo za watu wote na inamuweka mtu mbali na machafu. Kuonesha uso kunapelekea katika machafu na Hijaab kunamuwema mtu mbali na hilo. Na Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

“Na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika.”

Na “mapambo” ni yale yanayovutia kwa mwanamke; uso, nywele na yasiyokuwa hayo. Lililo la wajibu ni kuusitiri. Kwa kuwa uso ni fitina. Ni wajibu kuusitiri ili asiwafitinishe wengine. Ama Kauli Yake (Ta´ala):

 إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

“…  isipokuwa yale yanayodhihirika.”

Wameifasiri wanachuoni ya kwamba ni mavazi ya dhahiri ya kiada. Haya hakuna njia ya kuyasitiri na kuyaficha. Ni lazima yaonekane. Makusudio ya “mapambo” ni uso na yanayovutia kwa mwanamke; miongoni mwa nywele, mikono, miguu na kadhalika. Ama Athar ya Asmaa´ bint Abu Bakr, Hadiyth hii ni dhaifu. Kaipokea Abu Daawuud kwa isnadi dhaifu. Kwa kuwa imekuja kupitia njia Sa´iyd bin Bashiyr, Qataadah, Khaalid bin Burayq kutoka kwa ´Aaishah. Ni Hadiyth dhaifu na ina kasoro tatu… Na lafdhi sahihi ni kuwa, Asmaa´ bint Abu Bakr aliingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nyumbani kwa ´Aaishah, Mtume akamwambia: “Ewe Asmaa´! Mwanamke anapofikia umri wa kupata hedhi, asioneshe kitu isipokuwa hili na hili – akaashiria uso na vitanga.” Hadiyth hii iko wazi, lakini sio sahihi. Na ikiwa imethibiti basi itakuwa ni kabla ya Hijaab kuamrishwa. Kwa kuwa mwanamke kabla ya Hijaab kufaradhishwa alikuwa akionesha vitanga vyake na uso wake. Allaah alipofaradhisha Hijaab Akaamrisha kufunika. Lau khabari hii ni sahihi basi ilikuwa ni wakati wa hali ya mwanamke kabla Hijaab haijafaradhishwa, kisha Allaah ndio akaamrisha Hijaab ili kuwahifadhi na kuwalinda na sababu za fitina.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.youtube.com/watch?v=VU_qZrsezwA
  • Imechapishwa: 28/01/2024