al-Jahm na wafuasi wake wamewaita watu katika zile Aayah za Qur-aan na Hadiyth zinazotatiza, hivyo wakapotea na wakawapotosha watu wengi. Miongoni mwa mambo yaliyotufikia kutoka kwa al-Jahm, adui wa Allaah, ni kwamba alikuwa anatokea Tirmidh huko Khurasan. Alikuwa ni mtu wa magomvi na falsafa. Falsafa yake nyingi ilikuwa juu ya Allaah (Ta´ala). Akakutana na watu katika washirikina wakiitwa sama wasamani. Wakamjua al-Jahm na wakamwambia: ”Hebu tukuzungumzishe. Hoja zetu zikikushinda, basi utaingia katika dini yetu, na hoja zako zikitushinda, basi tutaingia katika dini yako”. Miongoni mwa mambo waliyomwambia al-Jahm ni: ”Wewe sunadai kuwa uko na mungu?” al-Jahm akajibu kwa kusema: ”Ndio.” Wakamuuliza: ”Wewe umekwishamuona mungu wako?” Akajibu: ”Hapana.” Wakamuuliza: ”Je, umeshayasikia maneno yake?” Akajibu: ”Hapana.”  Wakamuuliza: ”Je, umekwishanusa harufu yake?” Akajibu: ”Hapana.” Wakamuuliza: ”Je, umekwishamgusa?” Akajibu: ”Hapana.” Wakamuuliza: ”Utajuaje sasa kama uko na mungu?” al-Jahm akachanganyikiwa na hajui ni nani anayemwabudu kwa siku arobaini. Kisha na yeye akaja na hoja zilezile kama zinazotumiwa na mazanadiki wa kinaswara, nazo ni kwamba roho ilioko kwa ´Iysaa ni roho ya Allaah kutoka katika dhati ya Allaah; anapotaka kuumba kitu, basi Anaingia katika baadhi ya viumbe Wake na akazungumza kupitia ndimi za viumbe Wake ambapo akaamrisha na kukataza anayoyataka. Sambamba na hayo ni roho isiyoonekana. al-Jahm akachukua hoja kama hizo na akamwambia yule msamani: ”Wewe sunadai kuwa uko na roho?” Akajibu: ”Ndio.” Akamuuliza: ”Je, umekwishaiona roho yako?” Akajibu: ”Hapana.” Akamuuliza: ”Je, umekwishasikia maneno yake?” Akajibu: ”Hapana.” Akamuuliza: ”Umekwishaihisi?” Akajibu: ”Hapana.” Ndipo akasema: ”Basi vivyo hivyo Allaah hana uso unaoonekana, hana sauti inayosikika wala harufu inayonuswa. Si mwenye kuonekana na macho na hana maeneo maalum pasi na mengine.” Akatumia hoja kwa Aayah tatu zenye kutatiza:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.”[1]

وَهُوَ اللَّهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ

“Naye ndiye Allaah katika mbingu na katika ardhi.”[2]

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ

“Macho hayamzunguki bali Yeye anayazunguka macho yote.”

Akaijenga ´Aqiydah yake juu ya Aayah hizi, akaipindisha maana Qur-aan na akazikadhibisha Hadiyth za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akadai kuwa atakayemsifu Allaah kwa kitu katika yale aliyojisifu Mwenyewe ndani ya Kitabu Chake au kitu ambacho Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemsifia nacho, basi ni kafiri na wenye kufananisha. Matokeo yake akawapotosha watu wengi. Vilevile akafuatwa na wengi katika wafuasi wa Abu Haniyfah na ´Amr bin ´Ubaydah huko Baswrah. Dini ya Jahmiyyah ikawa namna hiyo[3].

[1] 42:11

[2] 6:3

[3] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 92-98
  • Imechapishwa: 22/04/2024