Mtu anapowauliza kuhusu maneno Yake Allaah (Jalla wa ´Alaa):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.”

wanajibu kuwa hakuna kitu mfano wake; Naye yuko chini ya ardhi ya saba kama alivyo juu ya ´Arshi. Hakuna maeneo anakosa kuwepo. Hawi maeneo fulani pasi po kwengine. Hakuzungumza na wala hatozungumza. Hakuna yeyote atayakayemuona duniani wala Aakhirah. Hasifiwi na wala hatambuliki kwa sifa. Hafanyi. Hana kikomo wala mwisho. Hafahamiki kwa akili. Yeye wote ni uso. Yeye wote ni ujuzi. Yeye wote ni usikizi. Yeye wote ni uoni. Yeye wote ni nuru. Yeye wote ni uwezo. Kwake hakuna mambo mawili. Hasifiwi kwa sifa mbili zinazotofautiana. Hana ujuu wala uchini, ukingo wala upande, wala kuliani wala kushotoni. Si mwepesi wala mzito. Hana rangi wala mwili. Hatambuliki wala kueleweka. Kila kinachokuingia akilini wa namna alivyo ni kinyume chake kabisa.

Tunaposema kuwa Allaah ni kitu, nao wanasema Yeye ni kitu lakini tofauti na vitu vyengine. Lakini kitu hicho ambacho si kama vitu vyengine, ndivo wanavomaanisha watu wenye busara. Hapo imebainika kwa watu ya kwamba hawaamini chochote, lakini wanaficha fedheha zao kwa yale wanayoyaonyesha hadharani.

Wanapoulizwa wanayemwabudu, wanajibu kwa kusema kuwa wanamwabudu Yule ambaye anawaendesha viumbe hawa. Huyu, ambaye anawaendesha viumbe hawa, hatambuliki na wala hana sifa zinazotambulika? Wakajibu kwa kuitikia ndio. Hivyo waislamu wamejua kuwa nyinyi hamuamini chochote. Mambo yalivyo ni kwamba mnaficha fedheha zenu kwa yale mnayoyaonyesha hadharani.

Tukiwauliza kama Huyu, ambaye anawaendesha walimwengu, ndiye ambaye alimzungumzisha Muusa (´alayhis-Salaam), wanajibu kuwa hazungumzi na wala hazungumzishwi, kwa sababu maneno hayawi isipokuwa kwa viungo vya mwili – na Allaah anakanushiwa kuwa na viungo vya mwili. Pindi mjinga anapowasikia maneno yao, basi hufikiria kuwa hakuna watu wanaomtakasa Allaah kama wao. Hata hivyo hajui kuwa nadharia yao inarejea katika upotofu na kufuru. Hahisi kuwa nadharia yao si lolote isipokuwa kumsemea uwongo Allaah[1].

[1] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 98-100
  • Imechapishwa: 22/04/2024