Swali: Kama inavyojulikana kwamba ni wajibu kujitenga na makafiri na kuwachukia, basi ni ipi hekima ya kuruhusiwa kuoa kutoka kwa watu wa Kitabu ilihali wao si miongoni mwa waumini ambao inatakiwa kuwachukia na bado kuna uhusiano wa kindoa kati ya mume na mke?

Jibu: Wanazuoni wametaja kwamba sababu ya hilo ni kuwa wao walikuwa ni watu wa Kitabu na wenye dini iliyo sahihi hapo awali, nayo ni dini ya Nabii Muusa na Haaruun na dini ya Nabii ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam), ambayo ni Uislamu. Walikuwa juu ya dini hiyo na walikuwa na Vitabu, ingawa wakabadilisha na kupotosha. Kwa hivyo wakakufuru kwa hilo na pia wakakufuru kwa kutomuamini Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa kuwa bado wana asili ya Kitabu – Tawraat na Injiyl – na walikuwa na dini waliyoitegemea ambapo wakipendana nayo na kuchukiana kwa ajili yake na wakilingania watu kwayo kwa madai yao, ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akaruhusu kuwaoa wanawake wao waliojiepusha na machafu, kwa maana wanawake waadilifu, wenye kujisitiri na kujiepusha na uchafu. Hata hivyo kuwaacha na kuoa wanawake waislamu ni bora zaidi kuliko kuwaoa wao. Hili ni ruhusa tu, si jambo bora zaidi. Dhahiri – na Allaah ndiye Mjuzi zaidi – ni kwamba sababu ya ruhusa hii ni kuwa asili ya dini yao ilikuwa ni yenye kuzingatiwa, tofauti na washirikina na waabudia moto ambao asili ya dini yao ni batili. Ama watu wa Kitabu asili ya dini yao ni ya mbinguni. Lakini walipoibadilisha na kuipotosha wakakufuru kwa matendo yao maovu. Vilevile Allaah alipomtuma Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakamkataa ndipo wakawa makafiri kwa hilo. Kadhlika walipomkataa Nabii ´Iysaa walipoteremshiwa wahy, mayahudi walikufuru kwa hilo. Lakini bado asili ya dini yao iliendelea kuwepo.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3443/الحكمة-من-اباحة-نكاح-الكتابيات
  • Imechapishwa: 06/09/2026