Hapa ndipo kichinjwa kimoja cha Udhhiya kinakutosha wewe na mzazi wako

Swali: Je, kichinjwa kimoja cha Udhhiyah kinanitosha mimi na baba yangu kwa sababu nimeoa na nina familia yangu na baba yangu pia ni vivyo hivyo?

Jibu: Ikiwa mnaishi katika nyumba moja, basi kichinjwa kimoja kinawatosheni. Sunnah hiyo inakuwa kwa ajili yako, baba yako, wakezo na watoto wako. Lakini ikiwa unaishi katika nyumba ya kujitegemea na baba yako anaishi katika nyumba ya kujitegemea, Sunnah ni kila mmoja achinje kwa ajili yake mwenyewe na watu wa nyumbani kwake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth… kwa sababu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akichinja kondoo wawili; mmoja kwa ajili yake na kwa ajili ya watu wa familia yake na mwingine kwa ajili ya ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa hiyo kwa kufupisha ikiwa kila mmoja katika nyinyi anaishi kwa kujitegemea, basi Sunnah ni kila mmoja achinje kwa ajili yake mwenyewe na watu wa nyumbani kwake. Lakini mkiwa mnaishi katika nyumba moja mmekusanyika na jambo lenu ni moja, kichinjwa kimoja kinatosha. Ni sawa pia mkichinja vichinjwa vingi. Jambo ni jepesi. Swahabah mtukufu Abu Ayyuub (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulikuwa wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tukichinja kondoo mmoja. Mtu anachinja kwa ajili yake na watu wa familia yake.”

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/11396/هل-تجزى-الاضحية-عن-الولد-المتزوج-وابيه
  • Imechapishwa: 10/06/2024