Hakuna dalili sahihi kwamba kumgusa mwanamke kunachengua wudhuu´

Swali: Je, kumgusa mwanamke kwa matamanio au pasi na matamanio, ni mamoja mke wake au mwanamke mwingine, kunachengua wudhuu´?

Jibu: Masuala haya wanazuoni wametofautiana. Maoni ya sawa ni kwamba hakuchengui wudhuu´. Ni mamoja amefanya hivo kwa matamanio au pasi na matamanio. Ni mamoja amemgusa mke wake au mwanamke mwingine muda wa kuwa hajatokwa na madhiy au kitu kingine. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwabusu baadhi ya wakeze kisha akaswali pasi na kutawadha. Isitoshe kimsingi ni kusihi na kusalimika kwa twahara. Kwa hivyo haijuzu kuichengua isipokuwa kwa kichenguzi kilichothibiti katika Shari´ah. Katika Shari´ah takasifu hakuna kinachojulisha kwamba wudhuu´ unachenguka kwa kule kugusa peke yake. Kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ

“… au mmewagusa wanawake… “[1]

Makusudio yake ni jimaa kutokana na maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Hayo yamesemwa na Ibn ´Abbaas na jopo la wanazuoni wengine. Makusudio yake sio kule kugusa peke yake. Makusudio yangelikuwa hayo basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angewabainishia Ummah. Kwani Allaah (Subhaanah) amemtuma hali ya kuwa ni mfikishaji na mfundishaji. Imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alikuwa akiwabusu baadhi ya wakeze kisha akaswali na hatawadhi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/137)
  • Imechapishwa: 22/08/2021