Hadiyth “Pindi mja anapogonjweka au kusafiri…”

Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

133 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

إِذَا مَرِضَ العَبْدُ أَوْ سَافَرَ كُتِبَ لَهُ مِثْلُ مَا كَانَ يَعْمَلُ مُقِيمًا صَحِيحًا

“Pindi mja anapogonjweka au kusafiri, basi ataandikiwa mfano wa yale aliyokuwa akiyafanya katika hali ya ukazi na uzima.”[1]

Ikiwa ni katika ada ya mtu kufanya matendo mema kisha akashikwa na ugonjwa na hakuweza kuyafanya, anaandikiwa ujira kamilifu. Himdi zote ni za Allaah kwa neema Zake. Kwa mfano ni katika ada yako kuswali na mkusanyiko [msikitini] kisha ukapatwa na maradhi na hukuweza kwenda kuswali na mkusanyiko, unaandikiwa kana kwamba umeswali na mkusanyiko. Unaandikiwa daraja ishirini na saba. Lau utasafiri na ni katika ada yako unapokuwa mkazi kuswali swalah zinazopendeza, kusoma Qur-aan, kuleta Tasbiyh, Tahliyl na Takbiyr, lakini uliposafiri safari ikakushughulisha na mambo haya, basi unaandikiwa yale uliyokuwa ukifanya katika mji wako katika hali ya ukazi.

[1]al-Bukhaariy (2996).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/189)
  • Imechapishwa: 28/08/2024