Hadiyth kusoma Basmalah kwa sauti zote ni dhaifu

Swali: Ni ipi hukumu ya kusoma Basmalah kwa sauti ya juu ndani ya swalah wakati wa kusoma Faatihah na Suurah nyenginezo?

Jibu: Wanazuoni wametofautiana juu ya jambo hilo. Baadhi yao wamependekeza hilo na wengine wamelichukiza na wakapendekeza kuisema kimyakimya, maoni ambayo yenye nguvu zaidi na bora. Imethibiti katika Hadiyth Swahiyh kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Niliswali nyuma ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alyhi wa sallam), nyuma ya Abu Bakr na nyuma ya ´Umar na hawakuwa wakisoma “Bismillaahi ar-Rahmaan ar-Rahiym” kwa sauti ya juu.”[1]

Zimepokelewa Hadiyth nyingi zikiwa na maana kama hiyo.

Imepokelewa katika baadhi ya Hadiyth yanayofahamisha juu ya kupendekeza kuisoma kwa sauti ya juu. Lakini hata hivyo ni Hadiyth ambazo ni dhaifu. Hatutambui Hadiyth Swahiyh na za wazi zinazojulisha juu ya hilo. Lakini jambo ni lenye wasaa na sahali. Haitakikani kugombana.

Hapana neno baadhi ya nyakati imamu akisoma Basmlah kwa sauti ya juu ili kuwajuza maamuma kwamba anaisoma. Lakini bora mara nyingi aisome kimyakimya kwa ajili ya kutendea kazi Hadiyth ambazo ni Swahiyh.

[1] Ahmad (12434), Muslim (399) na an-Nasaa´iy (907).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/119)
  • Imechapishwa: 15/10/2021