Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

112 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimuliaya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

أعْذَرَ الله إِلَى امْرِئٍ أَخَّرَ أجَلَهُ حَتَّى بَلَغَ سِتِّينَ سَنَةً

“Allaah humpa udhuru aliyemcheleweshea kufa kwake mpaka akafikisha umri wa miaka sitini.”[1]

Wanachuoni wamesema ya kwamba hampi udhuru anapofikisha muda huu. Husemwa mtu fulani ni mwenye kupewa udhuru anapokuwa kweli ni mwenye kustahiki hilo.

Maana yake ni kwamba Allaah (´Azza wa Jall) anapomwacha mtu mpaka akafikisha miaka sitini basi amemsimamishia udhuru. Amemsimamishia hoja na hana udhuru tena. Kwa sababu mtu ambaye Allaah amemwacha mpaka akafikisha miaka sitini anakuwa ni mwenye kujua katika Aayah na alama za Allaah kiasi cha kutosha na khaswa ikiwa kama amekulia katika mji wa Kiislamu. Ni jambo lisilokuwa na shaka juu ya kwamba hili linapelekea kwa mtu huyu kutokuwa tena na hoja akikutana na Allaah (´Azza wa Jall). Hana udhuru tena. Kwa mfano ikiwa kama alifanya upungufu katika umri wake ndani ya miaka kumi na tano mpaka ishirini, pengine tunaweza kusema kuwa ana udhuru.Kwa sababu alikuwa hajakomaa vizuri na kuzizingatia Aayah. Lakini Allaah akimbakisha mpaka miaka sitini hana udhuru tena. Huyu hoja imeshamsimamia.

Pomoja na kwamba hoja inamsimamia mwanadamu tokea pale anapobaleghe. Hapa ndipo ´ibaadah inamuwabijikia na hapewi udhuru kwa ujinga.

Lililo la wajibu kwa mtu ni yeye ajifunze katika Shari´ah ya Allaah yale anayoyahitaji. Kwa mfano akitaka kutawadha ni lazima ajue namna atakavyotawadha. Akitaka kuswali ni lazima ajue namna atakavyoswali. Akiwa na mali ni lazima ajue ni kiwango gani inakuwa wajibu kutoa zakaah na kadhalika. Akitaka kufunga ni lazima ajue namna atavyofunga na ni yepi yanayoharibu swawm. Akitaka kufanya hajj au ´umrah ni lazima ajue namna yake na ni mambo gani yamekatazwa katika ´umrah. Ikiwa ni mfanya biashara – kwa mfano ni mfanyabiashara wa dhahabu – ni lazima ajue ribaa, aina zake na mengineyo yote yanayohusiana nayo. Ikiwa ni muuza chakula ni lazima ajue namna ya kuuza chakula na nini maana ya kufanya ghushi na kadhalika.

Muhimu ni kwamba mtu anapofikisha miaka sitini hoja imemsimamia kikamilifu. Hana udhuru wowote. Ni lazima kwa kila mtu kujifunza Shari´ah yale anayoyahitajia; kuhusu swalah, zakaah, swawm, hajj, biashara na mengineyo. Mtu ajifunze kwa kiasi na anavyohitajia.

[1] al-Bukhaariy

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/140-142)
  • Imechapishwa: 28/04/2024