Ganzi na dawa zinazokuwa na vileo

Swali: Ni ipi hukumu ya kujitibu kwa vitu vya haramu? Je, dawa za ganzi na baadhi ya vileo vinavyopatikana katika baadhi ya dawa vinachukuliwa kuwa haramu? Je, inajalisha kama kuna dharurah au hakuna dharurah?

Jibu: Ni haramu na haijuzu kujitibisha kwa haramu. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Allaah hakujaalia shifaa ya ummah huu katika vile alivyowaharamishia.”[1]

Jengine ni kwamba Allaah hatuharamishii kitu isipokuwa ni kutokana na madhara yake. Kamwe kitu chenye madhara hakigeuki kuwa chenye manufaa. Hata kama baadhi watasema kuwa eti ni dharurah, hakuna dharurah ya kujitibisha kabisa. Mtu anaweza kujitibisha na asipone, kama ambavo mtu anaweza kupona pasi na kujitibisha. Kwa hivyo hakuna dharurah ya kujitibisha. Lakini ikiwa mtu anachelea kuangamia endapo hatokula nyamafu au nguruwe basi itafaa kwake kufanya hivo. Asipofanya hivo anakufa.

Kama tulivyosema hakuna udharura katika kujitibisha. Isipokuwa ikiwa kama kukatwa baadhi ya viungo vya mwili wakati wa dharurah. Ni jambo linalotambulika kwamba kukata viungo ni haramu, hata kama ni ncha ya kidole chake. Lakini kwa mfano mtu anapatwa na kansa na madaktari wakamshauri kwamba njia pekee ya kusitisha kansa hiyo ni kwa kukata kiungo fulani, basi kukata huko kunakuwa ni dharurah kunapokuwa na uhakika kwamba ukataji wa kiungo ndio kusita kwa maradhi hayo.

Kuhusu ganzi, haina ubaya wowote kwa sababu sio ulevi. Ulevi ulioharamishwa ni ule unaopelekea kupoteza akili kwa njia ya kuhisi ladha, hivyo sivyo inapokuja katika ganzi. Kwa ajili hiyo wanazuoni wanasema kuwa ganzi haina neno.

Kuhusu vileo vinavyopatikana katika baadhi ya dawa, ni haramu ikiwa vinalewesha. Na ikiwa athari haionekani na kumefanywa tu dutu ya pombe ili kuihifadhi dawa hiyo, basi hapana vibaya kwa sababu pombe hiyo haina athari yoyote.

[1] al-Bayhaqiy (10/5).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/30-31)
  • Imechapishwa: 10/07/2026