Swali: Baadhi ya wanazuoni wametoa fatwa zinazojuzisha kuingia bungeni. Unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Hili ni kosa. Fatwa ya Ibn Baaz ni ya makosa. Aliyeko hapa amfikishie asiyekuweko. Fatwa ya Ibn ´Uthaymiyn ni ya makosa. Fatwa ya Shaykh al-Albaaniy amewaruhusu waalgeria peke yao. Je, kuna Aayah au Hadiyth inayosema kuwa kupiga kura ni haramu isipokuwa tu nyinyi waalgeria? Hapana. Shaykh al-Albaaniy kuwaruhusu waalgeria ni makosa. Mi najua kuwa al-Ikhwaan al-Muslimuun upesi sana wataenda na kaseti hii kwa Shaykh Ibn Baaz na Shaykh Ibn ´Uthaymiyn. Hatukai hapa kwa ajili ya kumpaka mafuta yeyote.

Kuhusu Shaykh Ibn Baaz, Shaykh Ibn ´Uthaymiyn na Shaykh al-Albaaniy, ni kwamba pindi mwanachuoni anapokosea kosa moja ilihali ana mazuri mengi, basi kosa hilo linafunikwa na zile fadhilah zake. Hivo ndivo wanavosema wanazuoni. Mimi nina uhakika wamemwagiza mtu mwenye ndevu zinazofika kwenye kitovu kwa Shaykh Ibn Baaz na udhahiri wake anaonekana ni mtu wa Sunnah. Kisha mtu huyu anamuuliza Shaykh ni vipi tutawaachia nafasi wakomunisti na kwamba wakomunisti watatuzuia kulingania kwa Allaah na kutufukuza kutoka nje ya nchi – kama walivyonambia mimi – ambapo anawasadikisha. Fatwa hii ni ya kimakosa. Hatutakiwi kufuata kichwa mchunga. Hatukubali chochote kile kutoka kwa Shaykh Ibn Baaz, Shaykh Ibn ´Uthaymiyn wala Shaykh al-Albaaniy isipokuwa kitu chenye dalili kutoka ndani ya Qur-aan na Sunnah.

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.muqbel.net/fatwa.php?fatwa_id=1884
  • Imechapishwa: 18/08/2022