Swali: Ni ipi hukumu ya kuomba du´aa katika sehemu ya Multazam na kushikilia pazia ya Ka´bah?

Jibu: Kuomba du´aa katika Multazam hakuna tatizo. Jambo hili limefanywa na baadhi ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Imepokewa pia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilifanya, ingawa kuna udhaifu katika kusihi kwake. Lakini kwa kuwa limefanywa na baadhi ya Maswahabah. Kusimama pale kati ya nguzo na mlango wa Ka´bah na kuomba du´aa ni jambo linalokubalika. Kuna matarajio ya kuitikiwa du´aa.

Ama kuhusu kushikilia pazia ya Ka´bah hatujui dalili yoyote ya Kishari´ah inayothibitisha hilo. Jambo hili halina msingi. Kinachojulikana katika Sunnah ni kile alichokifanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa ndani ya Ka´bah; aliweka kifua chake na mikono yake katika ukuta wa ndani na akamwomba Mola wake na akaleta Takbiyr. Imepokewa hivyo na Usaamah bin Zayd na Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhum) kwamba alizunguka ndani ya Ka´bah, akaleta Takbiyr na kuomba du´aa. Aidha imepokelewa kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kupitia masimulizi ya Bilaal kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali Rak´ah mbili ndani ya Ka´bah. Hayo ndiyo yaliyothibiti. Lakini kutoka nje ya Ka´bah, hakuna dalili inayothibitisha kushikilia pazia, isipokuwa upande wa Multazam ambapo aliomba du´aa kunajuzu.

Akiomba du´aa katika sehemu yoyote ya Haram hakuna tatizo. Lakini kushikilia pazia ya Ka´bah kwa dhana ya baraka, hilo halina msingi. Hatujui msingi wowote wa hilo.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1106/حكم-الدعاء-في-الملتزم-والتشبث-باستار-الكعبة
  • Imechapishwa: 25/01/2026