Du´aa nyepesi ya kusoma katika Twawaaf

Swali: Katika maeneo ya Twawaaf na Sa’y kuna watu wanaochukua vijikaratasi na kuvisoma kwa sauti ya pamoja. Je, hili linafaa?

Jibu: Bora ni mtu kumwomba Mola wake peke yake, baina yake na nafsi yake, bila kuwasumbua wengine. Ikiwa mtu ana kitabu au kijikaratasi, basi anaweza kusoma mwenyewe bila kuwachanganya wanaofanya Twawaaf. Ikiwa itawezekana mtu kusoma mwenyewe kutoka kwenye kijikaratasi alicho nacho au kutoka kwenye kile alichohifadhi, ayasome kimyakimya kuliko kuwashawishi watu. Inatosha kusema:

سبحان الله، والحمد لله، ولا إله إلا الله، والله أكبر، ولا حول ولا قوة إلا بالله

”Allaah ametakasika na mapungufu, himdi zote njema ni za Allaah, hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, Allaah ni mkubwa na hapana namna wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah.”

Ni kheri kubwa ikiwa atarudia maneno haya wakati wa Twawaaf. Vinginevyo. Pia anaweza kuomba kwa kusema:

اللهم اغفر لي، اللهم ارحمني، اللهم أعتقني من النار، اللهم اغفر لي ولوالدي، اللهم انصر دينك وكتابك وعبادك المؤمنين

”Ee Allaah, nisamehe! Ee Allaah, nihurumie! Ee Allaah, niache huru na Moto! Ee Allaah, nisamehe mimi na wazazi wangu! Ee Allaah, inusuru dini Yako, Kitabu Chako na waja Wako waumini!”

Aombe kwa wepesi na bila kujikalifisha.

Hapana haja ya du´aa nyingi zilizoandikwa ambazo huwafanya watu kushindwa kuzikita katika ´ibaadah yao wakati wa Twawaaf. Inatosha kitu kidogo cha utajo wa Allaah.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/24988/حكم-الدعاء-جهرا-من-كتاب-في-الطواف-والسعي
  • Imechapishwa: 20/01/2025