Chagua ufunge siku sita zozote za Shawwaal unazotaka

Swali: Je, inafaa kwa mtu kuchagua funga ya zile siku sita za mwezi wa Shawwaal au swawm ya siku hizi ina wakati wake maalum? Mtu akifunga swawm hii inakuwa ni faradhi kwake?

Jibu: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayefunga Ramadhaan kisha akaifuatishia [siku] sita za Shawwaal, basi anakuwa kama amefunga mwaka mzima.”[1]

Ameipokea Imaam Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Siku hizi sio mahsusi za mwezi. Bali atachagua siku anazotaka katika mwezi. Akitaka anaweza kuzifunga za mwanzo wake, katikati yake au za mwisho wake. Akitaka anaweza kuzitenganisha na akitaka anaweza kuzifululiza. Kuna wasaa katika suala hili. Akiziharakisha na akazifuatanisha mwanzoni mwa mwezi ndio bora. Kwa sababu kufanya hivo ni katika kuharakia katika kheri. Swawm hiyo haitakuwa faradhi kwake. Bali inafaa kwake kuiacha katika mwaka wowote. Lakini kuendelea kuzifunga ndio bora na kamili zaidi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Matendo yanayopendeza zaidi kwa Allaah ni yale anayodumu kwayo mwenye nayo, ijapo yatakuwa machache.”[2]

[1] Muslim (1164).

[2] Muslim (782).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (15/390)
  • Imechapishwa: 03/05/2022