Baadhi ya mambo yaliyopendekezwa katika ´iyd

Wakati wa swalah ya ´iyd unaanza pale linapochomoza jua kiasi cha mkuki. Huo ndio wakati ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali ndani yake. Wakati wake unaendelea mpaka pale ambapo jua linapinduka.

´Iyd ikija kutambulika baada ya kuwa jua limeshapinduka, basi watu wataswali kesho hali ya kuilipa. Abu ´Umayr bin Anas amesema:

“Ulifichikana kwetu mwezi mwandamo wa Shawwaal tukaamka asubuhi hali ya kuwa tumefunga. Akaja mpandaji [farasi] mwishoni mwa mchana ambapo wakashuhudia kuwa waliona mwezi mwandamo wakati wa jana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaamrisha wafungue siku yao na kesho watoke kwa ajili ya ´iyd yao.”

Ameipokea Ahmad, Abu Daawuud, ad-Daaraqutwniy ambaye amiefanya kuwa nzuri. Pia imesahihishwa na jopo la mahufadhi.

Ingelikuwa swalah ya ´iyd inaswaliwa baada ya kuwa limekwishapondoka, basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asingeichelewesha mpaka kesho.

Jengine ni kwa sababu kilichosuniwa katika swalah ya ´iyd ni mkusanyiko wa watu wote. Kwa hivyo ni lazima itanguliwe na wakati ambao watu wataweza kujiandaa kwa ajili yake.

Imependekezwa kutanguliza swalah ya ´Iy-ul-Adhwhaa na kuchelewesha swalah ya ´Iyd-ul-Fitwr. ash-Shaafi´iy amepokea upokezi ambao katika cheni ya wapokezi kuna Swahabah anayekosekana: “Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwandikia barua ´Amr bin Hamz:

“Iharakishe  [swalah ya] al-Adhwhaa, ucheleweshe [swalah ya] al-Fitwr na muwakumbushe watu. Fanyeni wakati wa kuchinja uwe mpana kwa kuitanguliza swalah katika [´iyd] al-Adhwhaa. Fanyeni wakati wa kutoa Zakaat-ul-Fitwr kabla ya kuanza kuswali Swalat-ul-Fitwr.”

Imependekezwa kula baadhi ya tende kabla ya kutoka kwenda kuswali swalah ya ´Iyd-ul-Fitwr na mtu asile katika ´Iyd-ul-Adhwhaa mpaka kwanza kuswaliwe. Buraydah amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hatoki siku ya ´Iyd-ul-Fitwr mpaka ale na wala hali siku ya ´Iyd-ul-Adhwhaa mpaka aswali kwanza.”

Ameipokea Ahmad na wengineo.

Shaykh Taqiyy-ud-Diyn amesema:

“Wakati Allaah alipotanguliza swalah kabla ya kuchinja pale aliposema:

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

”Basi swali kwa ajili ya Mola wako na [pia ukichinja] na chinja [kwa ajili Yake]!”[1]

na akatanguliza kuswali kabla ya kutoa zakaah pale aliposema:

قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّىٰ وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّىٰ

“Hakika amefaulu ambaye amejitakasa na akataja jina la Mola wake na akaswali.”[2]

ikawa imependekezwa kutanguliza swadaqah kabla ya kuswali katika ´Iyd-ul-Fitwr na kwamba kunachinja kunakuwa baada ya kuswali katika ´Iyd-ul-Adhwhaa.”

Imependekezwa kutoka mapema kwenda kuswali ´iyd ili apate kuwa karibu na imamu na pia mut apate fadhilah za kusubiri swalah na hivyo thawabu  zake ziwe nyingi.

Imependekezwa kwa muislamu kujipamba kwa ajili ya kuswali ´iyd kwa kuvaa nguo yake nzuri kabisa. Jaabir amesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa na juba akilivaa siku katika ´iyd mbili na siku ya ijumaa.”

Ameipokea Ibn Khuzaymah katika “as-Swahiyh” yake.

Pia al-Bayhaqiy amepokea kwa cheni ya wapokezi nzuri kwamba Ibn ´Umar alikuwa akivaa katika ´iyd mbili nguo yake nzuri kabisa.

[1] 108:02

[2] 87:14-15

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mulakhaswsw-ul-Fiqh (01/269-271)
  • Imechapishwa: 30/07/2020