السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

Umeuliza namna mtoto wenu atakavofunga katika nchi ambayo mchana wake ni masaa kumi na sita. Hakuna utatizi wowote. Jambo lililowekwa katika Shari´ah ni yeye kuanza kufunga pindi kutapopambazuka mpaka pale jua litakapozama. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[1]

Akila daku mwishoni mwa usiku na akaona kwa juu weupe wa alfajiri, basi atalazimika kujizuia kula. Asipoona basi anaruhusiwa kula mpaka pale atakapoona. Kwa sababu kimsingi ni kwamba usiku bado ni wenye kubaki. Na kama haiyumkiniki kuona weupe wa alfajiri kutokana na miangaza ya umeme, basi atendee kazi vile ambavo dhana yake kubwa inavompelekea. Akijua jana jua limechomoza wakati gani, basi ajizuie saa moja na nusu kabla ya kuchomoza kwake. Kwa sababu mara nyingi kuna saa moja na nusu kati ya kuingia alfajiri na kuchomoza kwa jua. Hili ndio jambo la lazima. Allaah akuhifadhini.

السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

1393-07-22

[1] 02:187

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/117)