Mlango wa tano: I´tikaaf na kuna masuala yafuatayo:

Suala la kwanza: Maana ya I´tikaaf na hukumu yake

1- Maana

I´tikaaf maana yake kilugha ni kulazimiana na kitu na kuizuia nafsi juu yake.

Maana yake kidini ni muislamu kulazimiana na msikiti kwa ajili ya kumtii Allaah (´Azza wa Jall).

2- Hukumu

Ni Sunnah na kumwabudu Allaah (Ta´ala). Amesema (´Azza wa Jall):

وَعَهِدْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ

“Tulichukua ahadi kwa Ibraahiym na Ismaa’iyl kwamba waisafishe Nyumba Yangu kwa wanaotufu na wanaofanya i’tikaaf na wanaorukuu na kusujudu.[1]

Aayah hii ni dalili juu ya usuniwaji wake mpaka kwa nyumati zilizotangulia. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ

“Na wala msichanganyike nao hali ya kuwa nyinyi ni wenye kukaa I’tikaaf  misikitini.”[2]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikaa I´tikaaf zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan mpaka Allaah alipomfisha[3].

Waislamu wameafikiana juu ya usuniwaji wake na kwamba na kwamba ni jambo lililopendekezwa. Haimlazimu mtu isipokuwa pale atakapojiwajibishia mwenyewe kama vile aweke nadhiri. Kwa msemo mwingine ni kwamba usuniwaji wa I´tikaaf umethibiti kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano.

[1] 02:125

[2] 02:187

[3] al-Bukhaariy (2020) na Muslim (1172).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 167
  • Imechapishwa: 30/04/2021