Aminini yale yenye kusadikisha yale yaliyo pamoja nanyi

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَآمِنُوا بِمَا أَنزَلْتُ مُصَدِّقًا لِّمَا مَعَكُمْ وَلَا تَكُونُوا أَوَّلَ كَافِرٍ بِهِ ۖ وَلَا تَشْتَرُوا بِآيَاتِي ثَمَنًا قَلِيلًا وَإِيَّايَ فَاتَّقُونِ

“Aminini yale Niliyoyateremsha yenye kusadikisha yale yaliyo pamoja nanyi na wala msiwe wa kwanza wenye kuyakanusha na wala msiuze Aayah Zangu kwa thamani ndogo na Mimi pekee nicheni.”[1]

Nayo ni Qur-aan ambayo ameiteremsha kwa mja na Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo amewaamrisha kuiamini na kuifuata. Hayo yanapelekea kumwamini yule aliyeteremshiwa. Akataja sababu yenye kuwafanya wao kuamini:

مُصَدِّقًا لِّمَا مَعَكُمْ

“… yenye kusadikisha yale yaliyo pamoja nanyi…”

Bi maana ni yenye kuafikiana nayo na wala si yenye kwenda kinyume wala kupingana nayo. Yakiwa ni yenye kuafikiana na vile Vitabu mlivyonavyo na si vyenye kwenda kinyume navyo, basi hakuna kizuizi cha kumwamini. Kwa sababu amekuja na yaleyale waliyokuja nayo Mitume wengine. Nyinyi ni wenye haki zaidi ya kumwamini na kumsadikisha kwa sababu ni watu wa Kitabu na wasomi. Isitoshe maneno Yake:

مُصَدِّقًا لِّمَا مَعَكُمْ

“… yenye kusadikisha yale yaliyo pamoja nanyi…”

ipo ishara kwamba msipomwamini, basi hayo yatakurudilieni nyinyi wenyewe na kuonesha kuwa pia mnakadhibisha yale mlionayo. Kwa sababu yale aliyokuja nayo ndio yaleyale aliyokuja nayo Muusa, ´Iysaa na Mitume wengine. Kwa hiyo kumkadhibisha ni kukadhibisha pia yale mlionayo. Ndani ya Vitabu mlivyonavyo zipo sifa za Mtume huyu aliyetajwa ndani ya Qur-aan hii na vinambashiria. Kwa hivyo msipomwamini basi mtakuwa mmekadhibisha baadhi ya yale yaliyoteremshwa kwenu. Mwenye kukadhibisha baadhi ya yale yaliyoteremshwa kwake basi amekadhibisha yote. Ni kama ambavo yule mwenye kumkadhibisha Mtume mmoja peke yake basi amewakadhibisha Mitume wote.

Pindi alipowaamrisha kumwamini akawakataza na kuwatahadharisha kinyume chake ambacho ni kumkufuru. Amesema:

وَلَا تَكُونُوا أَوَّلَ كَافِرٍ بِهِ

“… na wala msiwe wa kwanza wenye kuyakanusha.”

Bi maana kumkanusha Mtume na Qur-aan. Maneno Yake:

وَلَا تَكُونُوا أَوَّلَ كَافِرٍ بِهِ

“… na wala msiwe wa kwanza wenye kuyakanusha.”

Ni yenye nguvu zaidi kuliko:

ولا تكفروا به

“Na wala msimkanushe.”

Kwa sababu wao wakiwa ndio wa mwanzo kumkanusha basi watu watakimbilia kumkanusha na pia itakuwa ni kinyume ya kile kinachowapasa. Isitoshe watakuwa ni wenye kupata dhambi zao na dhambi za wale wenye kuwaigiliza baada yao.

[1] 02:41

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 41
  • Imechapishwa: 29/06/2020