Ameweka nadhiri ya kusoma al-Baqarah kila siku

Swali: Nilikuwa nauguza mgonjwa ambapo nikachelea maradhi yasije kuhama kwangu. Matokeo yake nikaweka nadhiri Allaah akiniponya na maradhi haya basi nitasoma Suurah “al-Baqarah” kila siku. Hivi sasa baadhi ya nyakati napata uzito wa kufanya hivo.

Jibu: Kama anahisi uzito ni nani ambaye alimuwajibishia nadhiri? Ni yeye mwenyewe ndiye kajiwabishia nadhiri. Kwa ajili hii lau watu wangelikuwa na busara au sahihi zaidi lau watu wangelielewa, basi kamwe wasingeliweka nadhiri. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza nadhiri na akasema kwamba haileti kheri yoyote. Sikiliza maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema kwamba haileti kheri. Tunafanya kitu ambacho hakileti kheri? Hapana. Kwa ajili hii Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amemili juu ya kuharamisha nadhiri. Ni mamoja iwe inahusiana na neema au janga. Imekatazwa na imechukizwa machukizo makubwa.

Kwa hivyo tunamwambia mwanamke huyu kwamba yeye mwenyewe ndiye kajiwabishia kujisomea al-Baqarah kila siku. Kusoma al-BaqaImaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiynrah kila siku sio jambo gumu. Unaweza kusoma nusu ya juzu mwanzoni mwa mchana, nusu ya juzu wakati wa swalah ya Dhuhr na nusu ya juzu wakati wa swalah ya ´Aswr ambapo ukakamilisha baada ya alasiri au wakati wa asubuhi. Hii ni rahisi. Kwa sababu al-Baqarah ni takriban juzu mbili na nusu. Msomaji anaweza kuzisoma ndani ya saa moja na robo. Ni rahisi. Ni wajibu kwake kutimiza nadhiri yake. Asipofanya hivo nachelea asije kuwa miongoni mwa wale ambao Allaah amesema juu yao:

وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُوا بِهِ وَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ

“Miongoni mwao wako waliomuahidi Allaah [kwamba]: “Akitupa katika fadhila Zake, basi bila shaka tutatoa swadaqah na tutakuwa miongoni mwa waja wema.” Alipowapa katika fadhila Zake, walizifanyia ubakhili bna wakakengeuka na huku wakipuuza.”[1]

Malipo yakawa yepi?

فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَىٰ يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُوا اللَّـهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ

“Basi akawapachika unafiki katika nyoyo zao mpaka siku watakayokutana Naye kwa vile walivyomkhalifu kwao Allaah kwa waliyomuahidi na kwa yale waliyokuwa wakikadhibisha.”[2]

Kwa hivyo tunamwambia dada muulizaji amtake msaada Allaah na asome al-Baqarah kila siku kama alivyoilazimisha nafsi yake kufanya hivo.

[1] 09:75-76

[2] 09:77

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (54) http://binothaimeen.net/content/1235
  • Imechapishwa: 10/07/2020