Amenuia kufunga baada ya kuingia alfajiri

Swali: Fajr imempambazukia na hakunuia isipokuwa baada ya kuchomoza alfajiri. Ni ipi hukumu ya funga yake ya siku hiyo?

Jibu: Ni lazima kwake kulipa siku hiyo ambayo imempitikia sehemu yake pasi na kunuia. Ramadhaan mtu anatakiwa kunuia kila siku kivyake. Kwa sababu kila siku ni ´ibaadah yenye kujitegemea na hivyo inahitajia nia. Kwa hivyo anatakiwa kila siku kunuia kufunga wakati wa usiku. Akipambazukiwa na alfajiri na hakunuia – kama hali ya dada muulizaji – na akanuia baada yake, basi swawm yake haikufungika juu ya faradhi ya Ramadhaan. Bali ni lazima kwake kulipa siku hiyo. Ni mamoja ameiacha nia kwa makusudi au kwa kusahau.

Lakini kama alinuia usiku lakini akafikwa na kitu katika kusahau au akafikwa na kitu katika shughuli na hivyo nia ikampotea – ijapo amekwishanuia – kitu hiki kilichozuka hakiathiri midhali hakubadilisha kutoka katika ile nia yake ya kwanza. Kitu kidogo kilichozuka hakiathiri nia. Kwa hiyo swawm yake ni sahihi. Isipokuwa kama atanuia nia nyingine ambayo itamwondoa katika funga yake ya siku hiyo. Katika hali hiyo ni lazima atie nia upya wakati wa usiku.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (02/389-390)
  • Imechapishwa: 21/03/2022