Amekumbuka amesahau Tashahhud katika Rak´ah ya tatu

Swali: Imamu akisimama katika Rak´ah ya tatu katika swalah ya Rak´ah nne na wakati alipokuwa anasimama akakumbuka kuwa amesahau Tashahhud. Je, inafaa kwake kurudi nyuma akaketi chini?

Jibu: Hili linahitajia upambanuzi:

Kama amekwishasimama kwa kunyooka, basi haifai kwake kurudi katika Tashahhud. Katika hali hii analazimika kusujudu sijda mbili za kusahau.

Kama hajasimama kwa kunyooka, basi inafaa kwake kurudi katika Tashahhud. Katika hali hii analazimika kusujudu sijda mbili za kusahau.

Hadiyth inasema wazi juu ya jambo hilo:

“Ataposimama mmoja wenu kutoka katika zile Rak´ah mbili na asiwahi kusimama kwa kunyooka, basi arudi na kuketi chini. Na akiwahi kusimama kwa kunyooka, basi asirudi na kuketi chini. Badala yake anatakiwa kusujudu sijda ya kusahau.”[1]

 Swali: Kama yuko karibu zaidi na kusimama?

Jibu: Hii ni falsafa ya ki-Hanafiyyah. Sisi hatuzungumzii jambo hilo. Sisi tunazungumzia ima amekwishasimama kwa kunyooka, au hajasimama kwa kunyooka. Kama amekaribia kusimama kwa kunyooka, hiyo ina maana kwamba hajasimama kwa kunyooka. Kama ameinuka na amekwishasimama kwa kunyooka, basi haifai kwake kurudi na kuketi chini. Lakini mtu ambaye kabla tu ya kuinuka akakumbuka na bado hajasimama kwa kunyooka. Basi katika hali hiyo amefanya vizuri na halazimiki kusujusu sijda mbili za kusahau. Ama kama amekwishasimama kwa kunyooka, basi haijuzu kwake kurudi katika Tashahhud. Katika hali hiyo akifanya hivo basi amefanya jambo baya. Na kama amefanya jambo baya basi katika hali hiyo analazimika kusujudu sijda mbili za kusahau.

[1] Ibn Maajah (1208) na Ahmad (18248). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (2/133).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (586) Dakika: 24:40
  • Imechapishwa: 01/01/2021