Ameamka kuswali Fajr kwa kuchelewa

Swali: Ni ipi hukumu ya ambaye ameswali Fajr baada ya kuchomoza jua kwa kushindwa kuamka mapema?

Jibu: Hapana shaka kwamba kitendo hichi ni haramu. Haijuzu kwa mtu kuchelewesha swalah nje ya wakati wake pasi na udhuru. Kulala ni udhuru muda wa kuwa mtu hajazembea. Mtu mtu amepitiwa na usingizi kwa sababu ya kuzembea kwa namna ya kwamba amelala kuchelewa na aidha hakuweka alamu ya kumwamsha au kumwomba mtu amwamshe, anapata dhambi. Kuhusiana na mtu ambaye sio mwenye kuzembea na mazowea yake ni kuamka ndani ya wakati lakini hata hivyo siku hiyo akashindwa kuamka mpaka jua likachomoza, basi ataswali Fajr kama kawaida. Ataanza kwa kutawadha, kisha aswali Sunnah kisha ndio aswali Fajr. Abu Qataadah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Usiku mmoja tulisafiri pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baadhi wakasema: “Si tungelipiga kambi, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Nachelea msije kupitiwa na usingizi kutokana na swalah.” Bilaal akasema: “Nitakuamsheni. Laleni.” Bilaal akaegemeza mgongo wake kwenye kipando chake cha mnyama ambapo usingizi ukamchukua. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaanza kumka na miale ya jua imeshachomoza. Akasema: “Ee Bilaal! Kipi ulichosema?” Akasema: “Sijapatapo kulala kama nilivyolala mara hii.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Allaah amezichukua roho zenu alipotaka na akakurudishieni nazo alipotaka. Ee Bilaal! Amkeni na uwaite watu kuja kuswali.” Akatawadha na wakati lilipochomoza jua akasimama na kuswai.”[1]

Muhimu ni kwamba mtu anapaswa kufanya kila awezacho – ikiwa ni pamoja na kuweka alamu au kumwomba mtu anayemwamini – ili aweze kuamka kuswali Fajr kwa ile namna iliyoamrishwa.

[1] al-Bukhaariy (595).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/26)
  • Imechapishwa: 16/06/2026