Ambaye ni vyema akihiji kila mwaka na ambaye si vyema kwake kufanya hivo

Swali 24: Namshukuru Allaah kuona kwamba mimi sikosi Hajj kila mwaka. Hata hivyo nimeambiwa na baadhi ya watu kwamba tendo langu hili ndani yake kuna kuwaudhi waislamu, kwa sababu ninawabana, pamoja na kwamba mimi nawafaidisha wanaokwenda pamoja nasi katika wanawake kwa kuwaelekeza na kuwaongoza. Ni zipi nasaha na maelekezo yako kwangu?

Jibu: Ninaona kwamba mwanamke huyu ambaye wanawake wananufaika naye kwa kuwaelekeza na kuwaongoza ahiji. Suala la kubana, ikiwa yeye habani basi wanabana wengine. Kwa hivyo ikiwa yuko katika kundi anawaelekeza na kuwaongoza wanawake, basi hakuna shaka kwamba Hajj yake ni bora zaidi kuliko kubaki kwake. Ama ikiwa ni miongoni mwa wanawake wa kawaida, basi sisi tunasema kwamba kumsaidia yule anayetaka kuhiji faradhi kwa mali ambayo atahiji nayo ni bora zaidi. Kwa sababu hakika mtu ikiwa amemsaidia ndugu yake katika ´ibaadah, basi ni kama ameifanya yeye. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yeyote aliyemsaidia mpiganaji basi amepigana, na yeyote aliyemrithia katika familia yake kwa wema basi amepigana.”[1]

[1] al-Bukhaariy (2843) na Muslim (1895).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (21/32-33)
  • Imechapishwa: 07/05/2026