Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah, Mwenye kushukuru, swalah na amani zimwendee mpendwa mpendwa Wake mwenye kushukuru, jamaa zake na Maswahabah zake mpaka siku ya kufufuliwa.

Ama baada ya hayo;

Kijitabu hiki kinaitwa ”Fath-ul-Ghafuur fiy Wadhw´-il-Aydiy ´alaas-Suduur”:

1 – Imaam Ahmad amesema katika “al-Musnad”: Yahyaa bin Sa´iyd ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan: Simaak ametuhadithia, kutoka kwa Qabiyswah bin Hulb, kutoka kwa baba yake, ambaye amesema:

”Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akigeuka upande wake wa kulia na upande wake wa kushoto na nikamuona akiweka mkono wake juu ya kifua chake.”

Yahyaa akaonyesha kwa kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto juu ya kifundo[1].

2 – Abu Daawuud amesema: Abu Tawbah ametuhadithia, kutoka kwa al-Haytham (Ibn Humayd), kutoka kwa Thawr, kutoka kwa Sulaymaan bin Muusa, kutoka kwa Twaawuus, aliyesema:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto, kisha anaufunga juu ya kifua chake akiwa ndani ya swalah.”[2]

3 – Ibn ´Abdil-Barr ameeleza katika “at-Tamhiyd” kwamba Twaawuus amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto, kisha anaifunga juu ya kifua chake akiwa ndani ya swalah.”[3]

4 – al-Bayhaqiy amesema: Abu ´Abdillaah al-Haafidhw ametukhabarisha: ´Aliy bin Hamshaadh al-´Adl ametukhabarisha: Hishaam bin ´Aliy na Muhammad bin Ayyuub wametukhabarisha: Muusa bin Ismaa´iyl ametuhadithia: Hammaad bin Salamah ametuhadithia, kutoka kwa ´Aaswim al-Jahdariy, kutoka kwa ´Uqbah bin Suhbaan, kutoka kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesema kuhusiana na maneno Yake (Ta´ala):

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

”Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako!”[4]

”Kwa maana weka mkono wako wa kulia juu ya mkono wako wa kushoto ndani ya swalah.”[5]

Hivyo ndivyo alivyosema Shaykh wetu: Kutoka kwa ´Aaswim al-Jahdariy, kutoka kwa ´Uqbah bin Suhbaan.

5 – al-Bukhaariy amesimulia katika “at-Taariykh al-Kabiyr” kutoka kwa´Uqbah bin Dhwibyaan, kutoka kwa ´Aliy kuhusiana na maneno Yake Allaah (Ta´ala):

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

”Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako!”

”Aliweka mkono wake wa kulia juu ya katikati ya mkono wake wa kushoto, juu ya kifua chake.”

6 – Amesema: Abu Bakr Ahmad bin Muhammad bin al-Haarith al-Faqiyh ametukhabarisha: Abu Muhammad bin Hayyaan Abush-Shaykh ametukhabarisha: Abul-Huraysh al-Kilaabiy ametuhadithia: Shaybaan ametuhadithia: Hammaad bin Salamah ametukhabarisha: ´Aaswim al-Jahdariy ametukhabarisha, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa ´Uqbah bin Suhbaan, ambaye amesema:

”Wakati wa Aayah:

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

”Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako!”

´Aliy aliweka mkono wake wa kulia juu ya katikati ya mkono wake wa kushoto, kisha akaweka mikono hiyo juu ya kifua chake.”

[1] Ahmad (5/226).

[2] Abu Daawuud (759). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (759).

[3] at-Tamhiyd (20/75).

[4] 108:02

[5] al-Haakim (2/537).

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Hayaah as-Sindiy (afk. 1163)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath-ul-Ghafuur fiy Wadhw´-il-Aydiy ´alaas-Suduur, uk. 23-32
  • Imechapishwa: 07/05/2026