07. Uharamu wa picha ni wenye kuenea na unahusu picha aina zote

Hata hivyo bado kuna jambo linahitaji ubainifu, kwa sababu linaulizwa sana na wanazuoni wengi huliona kuwa ni tata. Nalo ni lile lililotajwa katika vitabu vya wanazuoni kuhusu sharti la kuwa sanamu iwe ya kiumbe hai kamili, iliyosimama yenyewe au iliyochongwa au iliyoshonwa – si iliyochapishwa tu.

Tambua ya kwamba kinachoonekana katika dalili ni kuzingatia ukamilifu, kwa sababu uharamu na adhabu iliyotajwa katika dalili pamoja na laana kwa watengeneza picha ni kwa kutengeneza picha za viumbe hai. Maana halisi ya hilo ni kuwa picha iwe ni ya mnyama kamili, kwa sababu anayechora sehemu ya mnyama haisemwi kuwa amechora mnyama, bali ni sehemu ya mnyama. Adhabu imekuja kwa kuchora mnyama kamili. Lakini ni lazima pia kuzingatia yale waliyoyataja wanazuoni, nayo ni kwamba ikiwa sanamu imekosa baadhi ya sehemu ambazo maisha ya mnyama hayawezi kusimama bila hizo, basi hiyo si sanamu iliyo haramu. Kwa sababu si sanamu ya mnyama kwa uhalisia. Ama ikiwa sanamu imekosa baadhi ya viungo ambavyo mnyama anaweza kuishi bila hivyo na pia hupatikana kwa namna hiyo katika uhalisia – kama macho, masikio au mfano wake – basi ingawa imekosa baadhi ya viungo bado inahesabika kuwa ni mnyama kamili. Kwa sababu iko katika umbo la mnyama anayepatikana katika uhalisia.

Kipimo katika kila aina ya wanyama kinategemea aina aliyokusudia mtengeneza picha kuichora. Hivyo kama atachora umbo la nusu mtu akikusudia kiumbe anayeitwa nasnaas ambaye baadhi ya wanahistoria wanasema yupo na ana umbo la nusu mtu, basi kuchora huko kunakuwa haramu ikiwa tutakubali kuwa kiumbe huyo yupo katika uhalisia. Hivyo zingatia mfano huu katika mifano mingine pia.

Ama kuzingatia kuwa picha iwe inasimama yenyewe, imechongwa, imeunganishwa kwa vipande na si yenye kuchapishwa, wamejengea dalili juu ya msimamo huo kwamba Zayd bin Khaalid – mpokezi yuleyule wa Hadiyth iliyotangulia kutoka kwa Abu Twalhah – alitembelewa na Bushr bin Sa´iyd katika kipindi ambacho alikuwa mgonjwa. Akakuta katika mlango wake kuna pazia lenye picha. Bushr akasema:

”Nikamuuliza ´Ubaydullaah al-Khawlaaniy: ”Je, Zayd si alitueleza kuhusu picha ile siku ya kwanza?” ´Ubaydullaah akajibu: ”Hukumsikia akisema ”Isipokuwa mchoro katika nguo”?”[1]

Namna hii ndivo ilivyopokelewa katika ”as-Sunan” ya Abu Daawuud na hiyo ni sehemu ya Hadiyth ya Abu Twalhah iliyotangulia. Vilevile wameipokea wengine kama ilivyotangulia.

Lakini haifichiki kuwa masimulizi haya ya Zayd bin Khaalid ni lazima ithibitike kuwa yamesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia njia ya Abu Twalhah. Ikiwa yamesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi inapingwa na Hadiyth iliyotangulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamuru ´Umar afute kila picha iliyokuwemo ndani ya Ka´bah – jambo la kufuta halitokei isipokuwa kwa kile kilichochapwa au kuchorwa – na mfano wake ni Hadiyth ya Ibn ´Abbaas iliyotangulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliamuru picha zilizokuwemo ndani ya Nyumba zifutwe. Katika hilo pia zimo Hadiyth Swahiyh zinazothibitisha uharamu wa tengeneza picha, kwani maana yake ya dhahiri ni ya jumla na hivyo inajumuisha zilizochapwa na zisizochapwa. Hivyo wajibu ni kubaki juu ya yale yanayolazimishwa na dalili hizi za jumla mpaka ithibitike kuwa maneno ya Zayd bin Khaalid yamesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa namna inayoweza kusimamisha hoja.

[1] al-Bukhaariy (3322) na Muslim (2106).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin ´Aliy ash-Shawkaaniy (afk. 1250)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Hukm-ut-Taswwiyr, uk. 31-35
  • Imechapishwa: 07/05/2026