Swali: al-Khadhir akiwa ameshakufa kwa dalili ya maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا جَعَلْنَا لِبَشَرٍ مِّن قَبْلِكَ الْخُلْدَ ۖ أَفَإِن مِّتَّ فَهُمُ الْخَالِدُونَ

”Hatukujaalia kwa mtu yeyote yule kabla yako aishi milele. Je, basi ukifa wewe wao watadumishwa milele?” (al-Anbiyaa´ 21:34)

Je, ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yeye anakuwa ameshakufa kwa kutumia dalili ya Aayah hiyohiyo?

Jibu: Kumepokelewa dalili zinazofahamisha kwamba ´Iysaa yuko hai. Ni jambo maalum. Kuhusu al-Khadhir hakuna dalili kwamba yuko hai. Ziko wapi dalili juu ya kwamba yuko hai? Hakuna dalili. ´Iysaa anatoka katika ujumla wake. Kwani ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) dalili zimefahamisha kwamba atateremka mwishoni mwa zama za mwisho akiwa hai, ahukumu kati ya watu, amuue ad-Dajjaal na ahukumu kwa Shari´ah ya Uislamu. Baada ya hapo na yeye pia afe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Si kwamba na yeye ataishi milele. Atakufa baadaye. Maneno Yake:

إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ

“Ee ‘Iysaa! Hakika Mimi ni Mwenye kukuchukua na Mwenye kukupandisha Kwangu.” (Aal ´Imraan 03:55)

haina maana ya kufa. Maana yake ni kwamba Malaika walimchukua na wakampandisha juu mbinguni. Ni kufa kuliko na maana ya kuchukuliwa. Imesemekana vilevile ´kufa` hapa maana yake ni amesinzizwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu kusinzia kuna maana pia ya kufa. Baada ya hapo akapandishwa juu mbinguni. Kwa ajili hii ndio maana akasema (Ta´ala):

وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ

“Hakuna yeyote katika Ahl-ul-Kitaa isipokuwa atamwamini kabla ya kufa kwake.” (an-Nisaa´ 04:159)

Ni lini hapa? Ni katika zama za mwisho. Watamwamini pindi atakapoteremka. Atavunja msabala, ataondosha kodi na hakutobaki isipokuwa tu dini ya Uislamu. Watamwamini kabla ya kufa kwake. Hii ni dalili kwamba katika zama za mwisho atakufa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam (09) http://ajurry.com/safrawy/chorohat-elakida/chorohat-nawakid-elislam/charh-salah-fawzan/09.mp3
  • Imechapishwa: 05/04/2019