al-Fawzaan kuhusu Takfiyr ya al-Hawaaliy na msemo wake “Swahwah”

Swali: Wako ambao wanaitwa “Mashaykh wa mwamko” na wanathibitisha katika darsa zao kwamba kuenea kwa maasi kama mfano wa nyukumbi za nyimbo, unywaji pombe na mfano wake ni dalili inayoonesha kuwa watu hawa wanayahalalisha, jambo ambalo ni kufuru kubwa[1]. Je, uthibitisho huu ni sahihi na unaafikiana na mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah?

Jibu: Kuhusu neno “mwamko” (Swahwah) limezuliwa. Anamaanisha kuwa waislamu walikuwa wamelala na hawakuamka isipokuwa hivi sasa? Ni nani mwenye kusema hivo. Waislamu bado ni wenye kuendelea kuamka juu ya dini yao. Hawakuamka hivi sasa, kama anavosema mtu huyu.

Kuhusu kukufurisha kwa maasi, haya ni madhehebu ya Khawaarij. Wao ndio wenye kukufurisha kwa maasi yaliyo chini ya shirki. Haifai kukufurisha kwa maasi yaliyo chini ya shirki. Lakini hata hivyo mwenye nayo ima ahukumiwe kuwa ni fasiki ikiwa dhambi yake ni dhambi kubwa au ni mtenda maasi ikiwa dhambi yake ni chini ya dhambi kubwa:

وَكَرَّهَ إِلَيْكُمُ الْكُفْرَ وَالْفُسُوقَ وَالْعِصْيَانَ

“Akakuchukizisheni kufuru na ufuska na maasi.”[2]

Kwa hiyo ngazi ni tatu; uasi, ufuska na kufuru. Haitakiwi kwa mtu kuwahukumu watu pasi na elimu wala yakini.

[1] Safar al-Hawaaliy amesema:

”Ipo hoteli nchi za Ghuba, Dubai, inayoitwa ”Hotel Metropotilan”. Katika hoteli hii kunasemwa waziwazi kwamba ipo pombe. Aidha zipo nyumba za majira ya joto, filamu za video na mengineyo. Ni mwaliko wa wazi kabisa. Walichukua mpaka picha kuthibitisha kwamba kunachezwa densi na wanawake wenye kuvaa vibaya wenye kutumia ulevi. Tunaomba ulinzi kwa Allaah dhidi ya kufuru hii. Hapana shaka kwamba ni kufuru kuhalalisha kitu ambacho Allaah amekiharamisha.” (Sharh at-Twahaawiyyah (2/272))

[2] 49:07

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/fathul%2004-07-1435-01.mp3 Tarehe: 1435-07-04/2014-05-04
  • Imechapishwa: 17/06/2020