Aadam na Hawaa wakiteremshwa ardhini

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

فَأَزَلَّهُمَا الشَّيْطَانُ عَنْهَا فَأَخْرَجَهُمَا مِمَّا كَانَا فِيهِ ۖ وَقُلْنَا اهْبِطُوا بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ ۖ وَلَكُمْ فِي الْأَرْضِ مُسْتَقَرٌّ وَمَتَاعٌ إِلَىٰ حِينٍ

“Shaytwaan akawatelezesha wote wawili kwayo ambapo akawatoa kutoka katika hali waliyokuwa nayo. Tukasema: “Shukeni hali ya kuwa maadui nyinyi kwa nyinyi na mtapata katika ardhi makazi na starehe hadi muda maalum.”[1]

Adui yao aliendelea kuwapambia yale waliyokatazwa kwa aina zake mbalimbali mpaka akawapelekea kuteleza kwa kuwapambia kwake:

وَقَاسَمَهُمَا إِنِّي لَكُمَا لَمِنَ النَّاصِحِينَ

“Naye akawaapia: “Mimi kwenu nyinyi wawili ni mwenye kukunasihini.””[2]

Matokeo yake wakadanganyika naye na wakamtii. Akawaondoa katika hali waliokuwa nayo ya kuneemeka na kujitanua na wakateremshwa katika nyumba ya uchovu na matatizo.

 بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ

“… hali ya kuwa maadui nyinyi kwa nyinyi.”

Bi maana Aadam na kizazi chake ni maadui wa Ibliys. Ni jambo linalotambulika kwamba adui siku zote hujitahidi kumdhuru yule adui yake, kumfikishia shari kwa kila njia na kumzuia na kheri kwa kila njia. Hapa kuna matahadharisho kwa wanadamu kutokamana na shaytwaan. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا ۚ إِنَّمَا يَدْعُو حِزْبَهُ لِيَكُونُوا مِنْ أَصْحَابِ السَّعِيرِ

“Hakika shaytwaan kwenu ni adui, hivyo basi mfanyeni kuwa ni adui. Hakika anaitia kundi lake ili wawe miongoni mwa watu wa Moto uliowashwa vikali mno.”[3]

أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا

“Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake kuwa marafiki badala Yangu na hali wao kwenu ni maadui? – ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu!”[4]

Kisha akasema:

وَمَتَاعٌ إِلَى حِينٍ

“… starehe hadi muda maalum.”

Mpaka utapomalizika muda wenu wa kuishi. Baada ya hapo mtatoka humo na kwenda katika nyumba ambayo mmeumbiwa kwayo na imeumbwa kwa ajili yenu.

Kuna faida kwamba wakati wa maisha haya umewekewa muda maalum. Kwa msemo mwingine sio makazi ya kihakika. Ni sehemu ya mtu kujizidishia matendo kwa ajili ya nyumba ya huko mbele na wala sio sehemu ya kuishi kwa utulivu.

[1] 02:36

[2] 07:21

[3] 35:06

[4] 18:50

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 40
  • Imechapishwa: 17/06/2020