99. Mashahidi wanaishi kwa Mola wao

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Mashahidi wako hai kwa Mola wao wanaruzukiwa.

MAELEZO

Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jama´ah ni kwamba mashahidi, nao ni wale waliouliwa katika njia ya Allaah kwa lengo la kufanya neno la Allaah liwe juu, wanaishi maisha ya kaburini ingawa maisha yao ya duniani yamekwishamalizika. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ

“Wala usiwadhanie wale waliouawa katika njia ya Allaah ni wafu, bali wahai, kwa Mola wao wanaruzukiwa.”[1]

وَلَا تَقُولُوا لِمَن يُقْتَلُ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتٌ ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ وَلَـٰكِن لَّا تَشْعُرُونَ

“Wala msiseme kwa waliouawa katika njia ya Allaah kuwa ni wafu, bali wakohai lakini hamhisi.”[2]

Hamuhisi kuishi kwao. Kwa sababu ni maisha ya ndani ya kaburi na ni miongoni mwa mambo ya Aakhirah na mambo yaliyofichikana. Sisi tunaamini kuwa wako hai lakini sio kama uhai wao wa duniani. Kwa ajili hiyo ndio maana mirathi yao hugawanywa na wake zao hukaa eda ya kufiliwa. Uhai wao baada ya kufa ni uhai wa kaburini.

Wale wenye kuuliwa katika njia ya Allaah walengwa ni wapambanaji kwa ajili ya kufanya neno la Allaah liweze kushinda. Hawa ndio mashahidi. Kuna bwana mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumuuliza mtu ambaye anapigana kwa ajili ya kasumba, ushujaa na kwa ajili ya kutaka kuonekana – ni nani katika hawa ambaye anapambana katika njia ya Allaah? Akajibu:

“Yule mwenye kupambana ili neno la Allaah liweze kuwa juu huyo ndiye yuko katika njia ya Allaah.”[3]

Kupambana katika njia ya Allaah kuna vigezo vyake. Haifai kwa kila mmoja kubeba silaha, kuua au kulipua. Mapambano katika njia ya Allaah ni lazima yawe chini ya uongozi wa mtawala wa waislamu. Ima yeye mwenyewe aongoze kikosi au amteua ambaye anaweza kufanya hiyo kazi. Kutekeleza mapambano ni katika mambo yanayomuhusu mtawala. Waislamu wanatakiwa kupambana bega kwa bega pamoja naye, ni mamoja ni mwema au mwovu. Muda wa kuwa hajafuru basi amri yake ya kupambana inatakiwa kutiiwa. Ama kila mmoja kuleta vurugu na kulipua na kuua sio katika njia ya Allaah. Kufanya hivi ni uharibifu, kueneza ufisadi juu ya ardhi na fujo. Uislamu hauruhusu mambo hayo. Uislamu hauyakubali mambo hayo kwa sababu yanapelekea kumwagika kwa damu, kupoteza haki za watu na kuharibu mali. Mambo haya ni fitina, sio mapambano. Natija ni ipi baada ya hapo? Vurugu na kuharibu mali, kama mambo yanavyoshuhudiwa.

[1] 03:169

[2] 2:154

[3] al-Bukhaariy (2810) na Muslim (1904).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 75-76
  • Imechapishwa: 30/08/2021