100. Adhabu na starehe ndani ya kaburi

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Roho za wenye furaha ni zenye kubaki hali ya kuneemeshwa mpaka katika ile Siku watakayofufuliwa. Roho za wala maanganivu ni zenye kuadhibiwa mpaka siku ya Qiyaamah.

MAELEZO

Kuadhibiwa na kuneemeshwa ndani ya kaburi ni jambo limepokelewa kwa mapokezi mengi. Muumini huneemeshwa ndani ya kaburi lake. Hufunguliwa mlango wa Peponi ambapo akapata sehemu katika raha na neema zake. Kaburi lake hukunjuliwa kiasi cha upeo wa macho yake na hubaki hapo mpaka pale atakapofufuliwa na Allaah siku ya Qiyaamah. Baada ya hapo ndio anaingia Peponi.

Sio roho peke yake ndio huneemeshwa bali starehe zinakuwa juu ya roho na kiwiliwili. Hata kama kiwiliwili kimekwishateketea na kuwa udongo, hupata starehe au adhabu. Vyote viwili hupata ima starehe au adhabu, hivi ndivo wanavoonelea Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Sio roho peke yake ndio inahisi hali ya ndani ya kaburi.

Roho za wala maangamivu hubaki ndani ya kaburi ambapo roho na kiwiliwili vyote viwili vikaadhibiwa. Roho na kiwiliwili chake vyote viwili huadhibiwa na kuhisi maumivu. Roho ina mafungamano na kiwiliwili ndani ya kaburi. Inaweza hata kutengana na kiwiliwili kama atakavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Roho ina mafungamano yafuatayo na kiwiliwili:

1 – Ndani ya tumbo la mama baada ya kipomoko kupuliziwa roho ambapo kikaanza kuishi, kutikisika na kupata chakula.

2 – Baada ya kuzaliwa roho ina mafungamano na kiwiliwili mpaka wakati wa kifo.

3 – Wakati wa kulala, kwa sababu ulalaji ni kifo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَهُوَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُم بِاللَّيْلِ وَيَعْلَمُ مَا جَرَحْتُم بِالنَّهَارِ

“Naye Ndiye anayekufisheni usiku na anajua yale yote mnayoyafanya mchana.”[1]

4 – Ndani ya kaburi.

5 – Baada ya kufufuliwa. Haya ni mahusiano yasiyoachana na kamilifu. Baada ya hapo ima mtu akaingia Peponi au akaingia Motoni.

Haya ndio mafungamano ya roho na kiwiliwili, kwa mtazamo wa Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika “ar-Ruuh” – na Allaah juu ya kila jambo ni muweza.

[1] 6:60

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 76-77
  • Imechapishwa: 30/08/2021