Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Waumini watapewa mtihani na kuhojiwa ndani ya makaburi yao:

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ

“Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya duniani na Aakhirah na Allaah huwaacha kupotoka madhalimu; na Allaah anafanya akitakacho.”[1]

MAELEZO

Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuamini fitina, bi maana kuhojiwa, ndani ya kaburi. Maiti atahojiwa pale tu atapolazwa ndani ya kaburi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mja anapolazwa ndani ya kaburi lake na marafiki zake wakamwacha na akasikia nyayo za viatu vyao, hujiwa na Malaika wawili. Mmoja wao anaitwa Nakiyr na mwingine anaitwa Munkar. Watamkaza na kumwambia: “Mola wako ni nani? Dini yako ni ipi? Ni nani huyu ambaye alitumwa kwenu?” Muumini atathibitishwa na Allaah na atajibu jibu la sawa: “Allaah ndiye Mola wangu, Uislamu ndio dini yangu na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio Mtume wangu. Ametujia kwa dalili na uongofu ambapo tukamwamini na kumfuata.” Kafiri, au mnafiki, atasema: “Eeh, eeh. Sijui. Niliwasikia watu wakisema kitu na mimi nikakisema.” Atapigwa nyundo, lau mlima ungepigwa nayo basi ungeligeuka udongo. Atapiga ukelele wa hali ya juu utaosikiwa na viumbe wote isipokuwa tu majini na watu. Lau jini au mwanadamu angelisikia ukelele huo basi angelikufa.”[2]

Hapa roho inarudi kiwiliwilini. Mnafiki na yule mwenye mashaka ambaye aliishi duniani juu ya unafiki na juu ya mashaka atajibu kwamba hajui. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanayaamini haya. Hadiyth kuhusu adhabu ya ndani ya kaburi zimeyapokea mambo haya kwa wingi na hakuna waliyepinga isipokuwa Mu´tazilah na watumiaji akili ambao hutegemea akili yao. Hawa ndio wanaopinga adhabu ya ndani ya kaburi na wanazipuuza dalili zote. Hawaamini adhabu wala starehe za ndani ya kaburi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kumzika maiti alikuwa akisema:

“Mwombeeni msamaha ndugu yenu na mtakieni uimara; kwani hakika hivi sasa anahojiwa.”[3]

Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ

“Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya duniani na Aakhirah na Allaah huwaacha kupotoka madhalimu; na Allaah anafanya akitakacho.”

Kwa ajili hiyo Allaah amesema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu wanafiki:

وَلَا تُصَلِّ عَلَىٰ أَحَدٍ مِّنْهُم مَّاتَ أَبَدًا وَلَا تَقُمْ عَلَىٰ قَبْرِهِ ۖ إِنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَمَاتُوا وَهُمْ فَاسِقُونَ

“Wala usimswalie yeyote kabisa miongoni mwao akifa na wala usisimame kaburini kwake. Hakika wao wamemkufuru Allaah na Mtume Wake na wakafa hali wao ni mafasiki.”[4]

Amemkataza kusimama karibu na kaburi la mnafiki na kumuombea uimara na msamaha, jambo ambalo linajulisha kuwa ni sawa kusimama karibu na kaburi la muumini na kumuombea du´aa.

[1] 14:27

[2] Ahmad (4/287) na Abu Daawuud (4753). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Mishkaah” (131).

[3] Abu Daawuud (3221).

[4] 9:84

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 77-79
  • Imechapishwa: 30/08/2021